Bonanza la Pemba kuchochea utalii, urithi wa kiutamaduni

Pemba. Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Arif Abbas amesema bonanza la Pemba Tourisport and Cultural linaendelea kuwa kichocheo cha utalii na urithi wa kiutamaduni visiwani humo kutokana na kuhusisha michezo ya asili.

Abbas ameyasema hayo Novemba 27, 2024 katika ufunguzi wa bonanza hilo ambalo lilianza na mchezo wa mbio za ngalawa katika Wilaya ya Mkoani.

“Bonanza hili lilianzishwa mwaka 2018 kwa lengo la kukuza sekta ya utalii na urithi wa kiutamaduni wa Pemba pamoja na kuifungua Pemba katika utalii wa michezo na utamaduni, pia limekuwa jukwaa la kuonyesha utajiri wa tamaduni na michezo ya kipekee kama mashindano ya ngalawa, gwaride la punda, Triathlon, na Duathlon.

“Jambo jema ni kuwa mwaka huu bonanza limepata mwonekano wa kimataifa kwa kushirikisha mchezaji kutoka Kenya, hatua inayounga mkono dhamira ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ya kufungua Pemba kitaifa na kimataifa,” amesema Abbas.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani,  Hamad Omar Bakari, amesema kuwa bonanza hilo ni jukwaa muhimu la kulinda urithi wa Pemba na kukuza sekta ya utalii, huku akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu.

“Bonanza hili ni fursa ya kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuonyesha uzuri wa Pemba kwa dunia,”ameongeza DC Bakari.

Bonanza hilo la siku nne ni sehemu ya juhudi za kukuza utalii endelevu na kuimarisha urithi wa kisiwa hicho ambapo katika mashindani hayo ya Ngalawa mshindi wa kwanza alizawadiwa hundi ya million 1.5, mshindi wa pili kapata milioni 1 na mshindi wa tatu kupata 700 na kila mshiriki alipatiwa tanga jipya la ngalawa katika mashindano hayo.

Related Posts