Israel yaishambulia Hezbollah licha usitishwaji mapigano – DW – 28.11.2024

Kulingana na taarifa iliyotolewa na msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari, wanajeshi wa Israel jana waliwaua wapiganaji kadhaa wa Hezbollah katika eneo la kusini mwa Lebanon.

Uwepo wa wapiganaji  katika eneo hilo kulikiuka makubaliano hayo na Hagari amesisitiza kuwa “kila ukiukaji wa vifungu vya mkataba huo wa usitishaji vita, utajibiwa kwa mashambulizi. Vikosi vya Israel vimesema pia, vinawazuia watu kadhaa waliokuwa wakikaribia maeneo kusini mwa  Lebanon  ambako wanajeshi wa Israel wanaendelea kuweka kambi, ingawa wanatakiwa kuondoka kwa awamu kutokana na masharti muhimu ya mkataba huo wa kusitisha mapigano.

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFILPicha: Carl Court/Getty Images

Makubaliano hayo ya muda wa miezi miwili yameweka wazi kwamba kundi la Hezbollah linapaswa kuwaondoa wapiganaji wake katika eneo la kusini mwa Lebanon na kuelekea upande mwingine wa mto Litani, takriban kilometa 30 kaskazini mwa mpaka wa Israel na Lebanon. Wanajeshi wa Israel wanatakiwa pia kurejea nchini mwao. Jeshi la taifa la Lebanon kwa ushirikiano na walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL, ndio wenye jukumu la kulinda usalama katika eneo hilo la mpakani.

Soma pia: Hezbollah yatangaza “ushindi” dhidi ya Israel

Hata hivyo, maelfu ya Walebanon waliolazimika kuyahama makazi yao kufuatia vita kati ya Israel na Hezbollah wameanza kurejea makwao tangu jana yalipoanza kutekelezwa makubaliano hayo, na hivyo kukaidi maonyo kutoka majeshi ya Lebanon na Israel yaliyowataka kuepuka baadhi ya maeneo ya kusini ambako kabla ya kuanza kutekelezwa kwa makubaliano hayo jana Jumatano, Israel ilifanya oparesheni kubwa ya kijeshi na kuyalenga karibu maeneo 180 ya Hezbollah eneo hilo.

Watu 17 wauawa katika Ukanda wa Gaza 

Mpalestina akishuhudia uharibifu huko Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
Mpalestina akishuhudia uharibifu huko Gaza kufuatia mashambulizi ya IsraelPicha: Omar Ashtawy Apaimages/ZUMAPRESS/picture alliance

Israel imeendeleza hivi leo mashambulizi yake huko Gaza hasa maeneo ya katikati mwa Ukanda huo ambapo watu 17 wameripotiwa kuuawa, huku ikipeleka vifaru zaidi maeneo ya kaskazini na kusini mwa Gaza.

Soma pia: Israel yasitisha vita Lebanon na kuendelea kuishambulia Gaza

Wapalestina bado wana matumaini ya kuona vita vya Gaza vikimalizika kama anavyoeleza Amal Abu Hmeid.

“Natumai makubaliano ya kusitisha mapigano yatapatikana kama ilivyokuwa huko Lebanon. Nitaacha kila kitu, nitawachukua wachukua watoto wangu tu twende kwenye ardhi na nyumba yetu, nikaone walichotufanyia. Nataka kuishi kwa usalama, Mungu akipenda kutakuwa na suluhu, natumai mapigano yatasitishwa ili tuishi kwa utulivu kama tulivyokuwa hapo awali,” alisema mwanamke huyo wa Kipalestina.

Hata hivyo Israel haijazungumza chochote kuhusu mapigano yanayoendelea huko Gaza hasa yaliyofanyika usiku wa jana na mapema leo asubuhi.

Vyanzo: (APE, DPAE)

 

Related Posts