MASHABIKI wa Yanga wengi wanaonekana kwa tabu sana hapa kijiweni na wachache wenye nyoyo ngumu wamekuwa wanyonge sana sababu ya yote ni vipigo vitatu mfululizo ambavyo timu yao imepata.
Ilianza kufungwa bao 1-0 na Azam ambalo lilihitimisha rekodi yao ya kutopoteza mechi kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kushinda michezo nane mfululizo.
Baada ya hapo ikafungwa mabao 3-1 na Tabora United, matokeo ambayo yalisababisha timu hiyo ifikie makubaliano ya kuachana na Kocha Miguel Gamondi na kuamua kumchukua Sead Ramovic.
Hata hivyo, Ramovic naye alikaribishwa vibaya kwani mchezo wake wa kwanza, Yanga ilipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Al Hilal ikiwa ni mechi ya kwanza ya timu hiyo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Kuna mengi tunayaona na kuyasikia baada ya matokeo hayo na kama inavyofahamika katika soka letu, timu inapofungwa kila mtu anaongea lake, wengine watalaumu, kuna watakubali matokeo na wapo huamua kusapoti timu.
Kunapotokea hali kama hiyo, hakuna namna inayoweza kuirudisha timu kwenye mstari zaidi ya watu kuwa na mshikamano na kuendelea kutoa sapoti kwa kikosi badala ya kupiga miluzi mingi na kila mmoja kujiamulia analotaka kufanya. Mfano kuna video inaonyesha watu wakiwapiga wenzao waliokuwa wakitoa maoni baada ya mechi huku wengine wakitoa maneno ya kashfa na kejeli kwa wachezaji, kocha na viongozi.
Hapo wanakuwa hawajengi bali wanazidi kuibomoa nyumba ambayo tayari imeshapata ufa wakati walipaswa kuhakikisha wanauziba huo ufa kwa kuwa wamoja na kuhakikisha kila upande unatimiza majukumu yake vizuri.
Ukomavu wa kuhimili nyakati ngumu ambayo timu inapitia kwa sasa unapaswa kuwa silaha kubwa itakayoifanya Yanga irudi kwenye mstari vinginevyo itakuwa kama vita vya panzi ambavyo humpa furaha kunguru.