AKILI ZA KIJIWENI: Camara kipa acha Simba itambe

SIKU ile ambayo Simba ilifungwa bao 1-0 na Yanga kwenye Ligi Kuu, kipa Moussa Camara alilaumiwa sana kaifungisha kisa mpira aliotema uliunganishwa na Mudathir Yahya na kuipa bao pekee la ushindi vijana wa Jangwani.

Hata hivyo, kijiweni hapa wengi walikataa dhana Camara aliifungisha Simba kwa vile ukitazama vizuri ule mpira wa faulo ya Chama (Clatous) inaonekana ulikuwa unaeenda golini.

Baada ya zile lawama ungetarajia kuona Camara akiathirika kisaikolojia na kushindwa kucheza vizuri katika mechi zilizofuata, lakini mambo yamekuwa tofauti kwa kipa huyo raia wa Guinea.

Jamaa kosa lile la mechi ya Yanga ni kama lilimkomaza zaidi kwani kuanzia pale hadi sasa, amekuwa katika kiwango bora sana na ni lulu kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Guinea.

Simba ndiyo imefaidi sana ubora wa Camara kwani ameamua mechi muhimu na kuiwezesha timu hiyo kupata ushindi baadhi zikiwa ni za Ligi Kuu Bara na nyingine za Kombe la Shirikisho Afrika.

Ile mechi na Al Ahli Tripoli ya Libya katika muda ambao Simba ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1 tena dakika za mwishoni za mchezo, Camara aliokoa hatari moja ambayo wengi waliamini ingekuwa bao na aliupangua mpira uliokuwa ukienda wavuni na kuwa kona ambayo baada ya kupigwa iliokolewa na kuzaa bao la tatu la Simba.

Camara alisaidia Simba ipate pointi tatu muhimu katika mchezo dhidi ya Pamba baada ya kuokoa shuti lililokuwa likienda wavuni na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Juzi tena jamaa aliokoa hatari nne ikiwemo mkwaju wa penalti wa Onze Bravos ya Angola katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulinda ushindi wa bao 1-0 wa timu yake kwenye mechi hiyo.

Wakati Camara akifanya vizuri kumbuka Simba pia ina makipa wengine wazuri benchi ambao ni Aishi Manula, Ally Salimu, Ayoub Lakred, Hussein Abel na Ally Feruzi.

Related Posts