BAADA ya kufushudiwa michuano ya Ligi ya Kikapu ya Taifa (NBL), sasa macho na masikio yanarudi kwenye mwendelezo wa Ligi ya Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL) inayozikutanisha miamba miwili JKT na UDSM Outsiders.
Licha ya kutotangazwa rasmi kwa tarehe itakayopigwa fainali ya pili, Kamishina wa Ufundi na mashindano hayo, Haleluya Kavalambi alisema itatangazwa na kwa sasa timu zinaendelea kujiandaa kwa mchezo huo.
Katika mchezo wa kwanza wa fainali hiyo, JKT ilishinda kwa pointi 67-62 na kutapigwa michezo mitano ‘best of five play off’ na hadi sasa JKT inaongoza kwa 1-0 na ikishinda miwili ijayo itaibuka bingwa kwa ushidi wa 3-0.
Kwa upande wa UDSM, endapo itashinda itakuwa imefungana mchezo 1-1 na zitacheza michezo miwili mingine ya kuamua bingwa.
JKT inajivunia na wachezaji wake Emanuel Chacha, Jonas Mushi, Omari Sadiki, Jackson Brown na Joseph Tungu.
Kwa upande wa UDSM Outsiders ina wachezaji nyota wenye uwezo wa kufunga katika maeneo yote ya mitupo mitatu ‘three point’ ambao ni Tyrone Edward na Evance Davies na Mwalimu Heri.
Upande wa nafasi ya ulinzi ‘Power forward’ wanae Jimmy Brown mwenye uwezo wa kudaka mipira yote ya ‘rebound’ pamoja kuzuia ‘blocks’.