Mbeya. Wakati idadi ya vifo vilivyotokana na ajali vikiongezeka kufikia watatu katika ajali iliyotokea jana, wananchi jijini Mbeya wameshauri hatua za haraka za kuchukuliwa ili kuondokana na mzimu wa ajali za mara kwa mara huku Serikali ikitoa msimamo.
Jana Novemba 27, 2024 katika mteremko wa Simike eneo la Mbembela jijini Mbeya, ilitokea ajali iliyohusisha lori lililogonga magari mengine sita, bajaji nne na pikipiki moja.
Katika ajali hiyo, watu wawili walifariki papo hapo huku wengine 10 wakijeruhiwa na kupelekwa hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu zaidi ambapo mmoja amefariki dunia wakati akipatiwa huduma ya matibabu.
Hata hivyo, eneo hilo hilo limeonekana kugharimu zaidi maisha ya watu kwani mapema Juni 2024, lori lilifeli breki na kugonga gari aina ya Costal lililokuwa likitokea mkoani Songwe na kusababisha vifo vya watu 14 na kujeruhi kadhaa.
Mkazi wa Mbeya, Benjamin Deus amesema kutokana na mfululizo wa ajali katika mteremko huo, ni vyema serikali kuchukua hatua kupitia mradi wa ujenzi wa barabara za njia nne kuanzia maeneo hatarishi.
“Inaumiza sana kila muda kushuhudia ajali, tulishauri tangu ajali iliyoua watu zaidi ya 10, kwamba eneo hili na mengine korofi ndio yaanze kujengwa kabla ya kwingine,” amesema Benjamin.
Naye Victor John amesema zipo ajali nyingine ambazo hutokea eneo hilo bila kuripotiwa akieleza kuwa lazima kuwepo hatua za haraka kunusuru maisha ya watu.
“Kuna ajali nyingine zinatokea tunaziona eneo hili ikiwamo pikipiki, bajaji na gari lakini hazitangazwi, tunaomba juhudi za haraka kurekebisha eneo hili ili kunusuru maisha ya watu,” amesema Victor.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa haraka, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroad) Mkoa wa Mbeya, Masige Matari amesema kilichokuwa kimewakwamisha ni miundombinu katika eneo hilo ambapo kwa sasa tayari wamerekebisha.
“Leo asubuhi nimeongozana na wataalamu na mkandarasi kwenye hilo eneo na nimeelekeza ujenzi kuanza haraka, tulishindwa mapema kutokana na miundombinu iliyokuwapo ya mnara wa TTCL, umeme na maji,” amesema Matari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva na kwamba jeshi hilo kwa kushirikiana na mmiliki wa gari, linaendelea kumtafuta dereva huyo.
“Tunatoa rai kwa madereva kuwa makini na kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika,” amesema Kuzaga.