Tahadhari yatolewa matumizi ya dawa kuepuka usugu

Dar es Salaam. Wakati ugonjwa wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (Uvida) ukitabiriwa kuongoza kwa vifo duniani ifikapo mwaka 2050, Watanzania wametahadharishwa kuacha mienendo isiyofaa ya matumizi ya dawa holela ili kuepuka tatizo hilo.

Wakati tahadhari hiyo ikitolewa, takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha makadirio ya usugu wa vimelea dhidi ya antibaotiki ni asilimia 59.8 huku utafiti ukionyesha wengi hutumia antibaotiki bila ushauri wa daktari.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huo husababisha vifo vya watu milioni 1.2 kwa mwaka, likitabiri hadi kufikia mwaka 2030 unaweza kusababisha vifo vya watu milioni 10 kila mwaka.

Uvida husababishwa na matumizi ya dawa bila kufuata maelekezo ya wataalamu, kutomaliza dozi baada ya kupata nafuu.

Pia, husababishwa na kutoa dawa bila kufuata miongozo iliyowekwa pamoja na kutokuwa na mwamko wa jamii katika kupata chanjo zinazosaidia watu kutougua ili wasitumie dawa.

Hayo yamebainishwa na Mfamasia Richard Charles kutoka Hospitali ya Aga Khan wakati akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Novemba 28, 2024 kwenye warsha iliyoandaliwa na Hospitali ya Aga Khan yenye dhumuni la kuongeza uelewa kwa wataalamu wa afya kuhusu uvida.

Warsha hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya kuongeza uelewa dhidi ya usugu wa dawa ambayo huanza Novemba 24 hadi 28 kila mwaka.

“Pia, Uvida husababishwa na kutopatikana kwa dawa za kupambana na magonjwa hususani maeneo ya kazi hivyo kutomaliza dozi zao, matumizi holela ya dawa kwa wanyama, mifugo na viumbe hai wengine yanaweza kusababisha Uvida,” amesema. 

 “Uvida ni janga linalohitaji kuungana kwa pamoja ili kupambana nalo kama kauli mbiu ya mwaka huu isemayo: Elimisha jamii kuchukua hatua na kushriki kikamilifu katika kuhakikisha jitihada zinakuwa endelevu.”

Akitaja athari za Uvida, Charles amesema moja wapo ambayo ni kubwa ni kifo cha mgonjwa akiwa nyumbani, kukaa hospitali kwa muda mrefu na gharama za matibabu zinaweza kusababisha umasikini.

“Tunaamini ushirikiano wa Serikali wadau wa maendeleo, sekta binafsi mifumo imara ya kujikinga na maambukizi, uwezo wa kimaabara, upatikanaji wa dawa kwa wakati vikiimarishwa vyote hivi tutapambana na Uvida,” amesema.

Hata hivyo, juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika kupambana na Uvida ikiwamo Serikali kuanzisha kampeni mbalimbali za kukabiliana nao ikiwamo ‘Holela-Holela itakukosti.’

Kupitia kampeni hizo Serikali imekuwa ikihimiza watu kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kabla ya kutumia dawa kutokana na athari zake kama ugonjwa kujirudia rudia na kuchukua muda mrefu kupona, kuenea na kusambaa kwa vimelea sugu vya magonjwa dhidi ya dawa na ulemavu.

Katika hafla hiyo wamealikwa wadau wa maendeleo, madaktari na wataalamu wa maabara na wafamasia kwa ajili ya kuongeza uelewa kwao na kwa jamii.

Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Adonis Bitegeko amesema warsha hiyo ya Aga Khan imesaidia wataalamu kuelewa jitihada za kupambana na Uvida.

Aidha, amesema kwa upande wao TMDA imekuwa ikihakikisha dawa zinazoingia nchini zina ubora na zimesajiliwa ili kuwa na dawa bora kwenye soko pia kufanya ukaguzi ili kuepusha usugu wa dawa kwa watumiaji.

Related Posts