Tarime. “Niseme ni Mungu tu, sijui niliweza vipi kushikilia ule mti hadi watu walipofika na kuniokoa kwani hadi natoka pale binafsi nilikuwa sijielewi ingawa nilikuwa sijapoteza fahamu lakini sikuwa natambua chochote,” hivyo ndivyo anavyoanza kuelezea Moses Ngare Moses, kijana aliyenusurika kifo wakati ndugu zake tisa wakisombwa na maji kwenye tukio lilitokea usiku wa kuamkia Novemba 25, 2024.
Ajali hiyo ilitokea katika Mtaa wa Bugosi wilayani Tarime baada ya mto Mori uliopo jirani na makazi yao kujaa maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ambapo katika tukio hilo jumla ya watu tisa walisombwa na maji.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 28, 2024, Moses ambaye katika tukio hilo amempoteza mama yake mzazi, dada yake wadogo zake, shemeji pamoja na watoto wa kaka na dada zake amesema siku ya tukio wakiwa wamemaliza kula walikuwa ndani wakisikiliza muziki bila kujua nini kilichokuwa kinachoendelea huko nje.
Amesema ghafla walishtukia ukuta wa nyumba yao ukianguka na walipotoka nje ndipo walikuta eneo lote la makazi yao likiwa limezingirwa na maji huku wasijue nini cha kufanya.
Amesema baada ya kuwepo kwa hali hiyo kila mtu katika familia hiyo iliyokuwa na watu 11 wakati huo alianza kutafuta namna ya kujiokoa ambapo yeye pamoja na dada yake, na binti ambaye alikuwa ni mgeni wao siku hiyo waliruka kwenye maji na kuanza kutafuta namna ya kujiokoa.
“Tuliruka kwenye maji ambayo yalikuwa yanafika kwenye usawa wa magoti na yalikuwa na kasi sana tukajibanza kwenye uwazi uliokuwepo kati ya nyumba na jiko lakini maji yakizidi ndipo tukahangaika hadi kufika kwenye mti uliokuwepo pale nyumbani,” ameeleza.
Amesema baada ya kufika kwenye mti huo wakiwa watatu huku dada yake akiwa amembeba mtoto mkononi ndipo walipobaini kuwa amembeba vibaya mtoto hivyo akataka kumuweka vizuri ili aweze kushikilia mti.
“Hapo ndipo nilipomuona dada yangu na mtoto wake kwa mara ya mwisho kwani akiwa anamuweka mtoto wake vizuri aliteleza na kuchukuliwa na maji sikuwaona tena, na kuhusu mama yangu na watu wengine sikuweza hata kuwashuhudia namna walivyosombwa na maji kwani baada ya maji kuzingira mji kila mtu alitafuta namna yake ya kujiokoa nikajikuta nimebaki mimi na mgeni wetu,” anaeleza.
Amesema baada ya dada yake kusombwa na maji alijikuta akichanganyikiwa asijue nini cha kufanya huku akiwa anaendelea kushikilia mti yeye pamoja na mgeni wao na kwamba hata nguvu za kuendelea kushikilia mti huo hajui alizotoa wapi akiamini kunusurika kwake ni kwa muujiza wa Mungu pekee.
Kaka wa Moses, Joel Ngare amesema kutokana na tukio hilo familia yao imebaki na watu wawili pekee yaani yeye na mdogo wake aliyenusurika siku ya tukio, huku akieleza kuwa baba yao mzazi alifariki dunia Septemba 16, 2024 katika eneo hilo la Bugosi baada ya kuugua.
“Nasubiri nijue Serikali itafanya nini na kama ikishindikana basi itabidi nimchukue mdogo wangu niende naye Kenya ambapo ndipo ninapofanyia shughuli zangu kwani sina namna nyingine na tumebakia wawili tu,” amesema
Joel amesema baada ya kumzika baba yao Septemba 23 alirudi nchini Kenya kwenye shughuli zake huku akiwa na mpango wa kurejea nyumbani kwaajili ya kusalimia mama yake pamoja na wadogo zake hasa ikizingatiwa kuwa jukumu la malezi ya familia hiyo lilikuwa ni la kwake baada ya baba yao kufariki dunia.
Akizungumza wakati wa mazishi ya watu hao, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amewaagiza viongozi wa serikali na kimila katika wilaya zote za mkoa huo kushirikiana pamoja kuwaondoa watu wanaoishi mabondeni, kwenye mikondo ya maji na maeneo hatarishi ili kuepuka athari zaidi zinzaoweza kutokea.
Mtambi amesema ingawa tukio lililotokea ni la kusikitisha lakini linapaswa kuwa fundisho kwa wengine wanaoishi katika mazingira hatarishi.
“Kama elimu kwa njia ya kawada itashindikana basi ikibidi hata nguvu zitumike kwa nia njema kabisa kwani hatuko tayari kuona watu wanapoteza maisha wakati upo uwezekano wa kuepuka matukio kama haya na kuepuka ni kuhama kutoka katika mazingira hayo hatarishi,” amesema.
Mtambi ameziagiza wilaya zote kutumia mvua zinazoendelea kunyesha na kujua historia ya maeneo mbalimbali na kuweza kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi kuepuka maeneo hatarishi kutumika kama makazi ya watu.
“Tumepoteza mtoto mdogo kwasababu sisi wakubwa tumeshindwa kumlinda, tumesababisha kiumbe hiki kipoteze uhai wake kwasababu ya uzembe wetu, naomba hii hali isijirudie tena, tusisubiri hadi majanga yatokee tuchukue hatua mapema kuzuia,” ameongeza Mtambi.
Amesema mbali na serikali kugharamia mazishi ya watu hao lakini pia ofisi yake itatoa Sh1 milioni kama rambirambi kwa familia.
Mtambi pia amewataka wakazi wa mkoa huo hasa wanaolazimika kuvuka mito kwaajili ya shughuli mbalimbali kuwa na subira nyakati hizi za mvua pale wanapoona ongezeko la maji katika mito hiyo kusubiri hadi pale maji yanapokuwa yamepungua ndipo waweze kuvuka.
Amesema mwaka jana wakati wa msimu wa mvua wapo watu waliopoteza maisha kwa kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka mito huku mito hiyo ikiwa na ongezeko la maji badala ya kusubiri maji yapungue.
Wakati miili hiyo ya watu wanane ikizikwa katika makaburi ya pamoja eneo la Magena mjini Tarime, mwili wa mtoto Ochola Joel (1) bado haujapatikana licha ya jitihada za kuutafuta zilizofanywa na vyombo vya uokozi kwa kushirikiana na wananchi.
Tukio hilo lilihusisha familia mbili ambapo watu tisa wa familia moja iliyokuwa na watu 11 walisombwa na maji na watu wawili wakinusurika.
Familia ya pili iliyokuwa na watu tisa ilinusurika huku ikipoteza mali zote ikiwa ni pamoja na nyumba yao kusombwa na maji.
Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara umetoa msaada wa magodoro sita, sukari, mchele sabuni, maharage, mafuta ya kula kwa familia iliyonusurika pamoja na vifaa vya shule kwa wanafunzi wa familia hiyo.
Akikabidhi msaada huo, Ofisa Uhusiano wa Mgodi huo, Francis Uhadi amesema mgodi huo umeguswa na tukio hilo hivyo umeona kuna haja ya wao kushirki kwa kutoa msaada huo kwa familia hiyo ambayo imepoteza kila kitu kwenye tukio hilo.
“Tunajua hatuwezi kurudisha uhai lakini tumeona kuna umuhimu wa sisi kushiriki kuwapunguzia magumu waliyoanayo wenzetu kwa sasa tunaamini huu msaada kwa namna moja ama nyingine utawafaa kwa wakati huu,” amesema.