Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Shirika la Bahari Duniani (IMO), Antonio Dominguez ametaka kuwapo kwa juhudi za pamoja za kudhibiti uharamia wa meli unaoendelea katika maeneo mbalimbali.
Kufanya hivyo kutasaidia kurejesha amani katika usafirishaji wa bidhaa baharini, jambo litakalopunguza mzigo wa gharama kwa wafanyabiashara, ambazo mwisho wa siku husababisha ugumu wa maisha kwa wananchi.
Dominguez ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Novemba 28, 2024 katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa kutoka nchi zaidi ya 40 duniani, kuzungumzia namna ya kupambana na uharamia katika usafiri wa majini.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Dominguez amesema usalama wa baharini una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa dunia, kwani unabeba ustawi wa mazingira na jamii kote ulimwenguni.
Bila jitihada kufanyika katika kutokomeza suala hilo, amesema ni ngumu kupata bidhaa, huduma na hata misaada ya kibinadamu, ambayo ni muhimu kwa maisha ya mabilioni ya watu duniani.
“Tukizingatia mashambulizi yanayoendelea dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Sham yanahatarisha usalama wa wanamaji, utulivu wa biashara na usalama wa kanda. Ninakaribisha mbinu ya kamati ya uongozi katika kutafuta suluhisho la kikanda kwa changamoto hii ya dharura,” amesema.
Amesema hatua ambazo zimefanywa katika kuratibu shughuli kwa ushirikiano na washirika wa kimataifa, ni mfano unaohitajika katika kukabiliana na vitendo hivi vinavyoongezeka.
“Pia, ni lazima tuhakikishe juhudi hizi za pamoja zinaendelezwa na kuimarishwa ili kulinda njia zetu za baharini na kuepuka kurudi kwa ukosefu wa amani kama ilivyokuwa wakati wa migogoro ya uharamia hapo awali,” amesema.
Mbali na uharamia pia ameshauri uhalifu mwingine kutopuuzwa, ukiwemo ule wa magendo, uchafuzi wa bahari na biashara haramu ya binadamu na wanyamapori.
“Pia uwepo wa vitu vipya kama kama mashambulizi ya mtandaoni, matumizi ya ndege zisizo na rubani navyo vinahitaji tahadhari yetu ya mara kwa mara na hatua za pamoja,” amesema.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zilikuwa zikiathiriwa na uharamia unaofanywa katika maeneo mbalimbali ya bahari kutokana na kuongezeka kwa gharama za bidhaa.
Mfano, mfereji wa Suez Canal unakadiriwa kupitisha asilimia 10 ya biashara ya kimataifa na takribani asilimia 22 ya makontena yote.
Inaelezwa kuwapo kwa uharamia unaofanyika, watu wanapolazimika kubadilisha njia huongeza mahitaji ya meli za makasha kwa asilimia 12.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema changamoto ya uharamia iliyokuwapo katika eneo la Bahari ya Sham mwaka jana zilikuwa na athari kubwa.
Miongoni mwa athari hizo, ni watu kuuawa jambo ambalo liliweka wasiwasi na watu kulazimika kupita njia ya mbali, na hivyo kuongeza gharama za uendeshaji meli kwa kutumia mafuta mengi.
‘Jambo hili lilifanya bei za vitu ikiwemo vyakula na mafuta kupanda. Sasa ni wakati wa Serikali zote hasa katika ukanda wa Bahari ya Sham, Guba ya Aaden, Djibouti kuamua kuwa tunaweka mkakati wa kupambana na maharamia wa meli ili bahari iwe salama kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usafirishaji,” amesema Profesa Mbarawa.
Kufanya hivyo kunasaidia biashara kuwa nzuri na wananchi wanapata bidhaa zao kwa bei nafuu zaidi.
“Uharamia ukitokea hatupambani Tanzania pekee, bali tunasimama kama jumuiya kwa sababu wengine wana meli zinapita na sisi tunahitaji mahitaji yetu, sasa kadri uharamia unavyokuwa mkubwa hata meli mbalimbali haziwezi kufika na zile zitakazofanikiwa, bei za bidhaa itakuwa kubwa zaidi, ndiyo maana jambo hilo linafanyika,” amesema.
Amesema jumuiya yote ya nchi zilizopo maeneo hayo hushirikiana kupambana na maharamia kwa kushirikiana na meli za vita za Marekani ili kuweka urahisi katika mapambano hayo.
“Kilichopo ni kwamba kila teknolojia ikibadilika na wao wanakuja na mbinu mpya za uharamia, hivyo inailazimu jumuiya hii kukaa kila wakati kuangalia kilichofanyika kuona ni kwa kiasi gani kinahitaji maboresho,” amesema.