BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Halima Vunjabei ametoa zawadi ya mkanda wake wa ubingwa wa dunia WBF International kwa Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kumchakaza mpinzani wake Songuel Ayten raia wa Uturuki kwa Knockout ya raundi ya tatu nchini Ujerumani.
Vunjabei amekabidhi mkanda huo leo Novemba 28, 2024 kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa wakati alipokuwa akimkabidhi zawadi ya Sh5 milioni ya Knockout ya Mama.
Wikiendi iliyopita, Vunjabei aliweka rekodi mpya nchini katika mchezo wa ngumi za kulipwa ya kuwa mwanamke wa kwanza kushinda mkanda wa ubingwa nje ya nchi.
Akizungumza mara baada ya kutoa zawadi hiyo, Msigwa alimpongeza bondia huyo kwa kufanikiwa kuitangaza nchi huku akimataka kuendelea kuwatwanga wengine katika mapambano ya kimataifa.
“Kwanza hongera Halima kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa kutokana na kushinda mkanda wa WBF, lakini nataka kuona ukiendelea kupiga hatua nyingine ya kuleta mikanda zaidi.
“Naliagiza Baraza la Michezo la Taifa, mkae naye ili muone namna gani mnaweza kumsaidia kwa sababu tunahitaji kuona akileta mikanda mingi, nampa hii shilingi milioni tano ya Knockout ya Mama kutokana na kile ambacho amekifanya Ujerumani,” alisema Msigwa.
Kwa upande wa Vunjabei, ameishukuru BMT na Rais Samia Suluhu Hassan kwa zawadi ya Sh5 milioni huku akiomba mkanda wake alioshinda Ujerumani apelekewe Rais Samia.
“Naishukuru BMT, Kamisheni ya ngumi za kulipwa nchini na serikali kupitia Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa sapoti kubwa ambayo wanatupa, sina cha kumlipa mama lakini mkanda huu wa ubingwa naomba afikishiwe kama zawadi yangu kwake,” alisema.
Vunjabei mwenye umri wa miaka 29, mpaka sasa amefanikiwa kucheza mapambano 29 sawa na raundi 180 tangu alipoanza kucheza ngumi mwaka 2014.
Katika mapambano hayo, ameshinda 15 yakiwemo 9 kwa KO, huku akipoteza 13 ikiwemo KO moja na sare moja.