Aliyetimuliwa Yanga aipa ubingwa Zambia

ALIYEKUWA Kocha wa Yanga Princess, Charles Haalubono, amefanikiwa kuiongoza timu ya taifa ya Zambia ya wanawake chini ya miaka 20 kutwaa ubingwa wa mashindano ya COSAFA.

Zambia imetwaa ubingwa huo baada ya kuichapa Msumbiji bao 1-0 katika mchezo wa mwisho uliochezwa nchini Afrika Kusini.

Katika mashindano hayo, Haalubono aliiongoza Zambia kwenye mechi nne kushinda zote, huku timu yake ikifunga mabao 19 ikiwa haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.

Wakati Zambia ikiwa bingwa kwa kuongoza kundi na pointi zake 12, imefuatiwa na Afrika Kusini iliyomaliza na pointi 9, Msumbiji (4), Lesotho (2) na Botswana (1).

Kocha huyo raia wa Zambia, alidumu Yanga Princess kwa msimu mmoja akiiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Wanawake.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya ubingwa huo, Haalubono alisema kama kocha inatengeneza wasifu (CV) mzuri kwake na kuliwakilisha vyema taifa lake.

“Nashukuru tumechukua ubingwa, hii inanipa motisha ya kuendelea kupambana kama kocha, kikubwa zaidi taifa langu ambalo liliniamini na kunipa kazi ya kuiongoza timu hadi tunamaliza mashindano,” alisema Haalubono na kuongeza.

“Naweza kusema licha ya ubingwa lakini tuna kikosi kizuri ambacho kinaweza kufunga na wakati huohuo kujilinda, naamini kama wataendelea hivi basi tutapata wachezaji wengi kucheza ligi mbalimbali.”

Related Posts