Unguja. Zaidi ya kampuni 40 kutoka Ubelgiji zimefika Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta za nishati, kilimo, utengenzaji wa bidhaa, utalii, usafiri na usafirishaji.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Novemba 28, 2024 na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Umoja wa Ulaya, Jestas Nyamanga kwenye jukwaa maalumu la biashara na uwekezaji.
Jukwaa hilo ni kati ya Ubelgiji na Zanzibar ambalo limehusisha kampuni hizo, wafanyabiashara na mamlaka za uwekezaji Zanzibar.
“Nimekuja na ujumbe wa kampuni takribani 40 kutoka Ubelgiji ambazo zinataka kuangalia fursa katika maeneo hayo, ndiyo maana tunao hapa tunapata taarifa sahihi, baadaye watatembezwa katika baadhi ya miradi, ikiwemo Bandari ya Mangapwani ili waone fursa zipi za uwekezaji na sekta nyingine na uwekezaji kwa ujumla,” amesema.
Amesema wawekezaji wanaotoka mataifa ya nje wanaridhika na mabadiliko yanayofanywa na mazingira mazuri katika sekta za uwekezaji na biashara nchini Tanzania.
Amesema kuna zaidi ya miradi 40 kutoka Ubelgiji iliyowekezwa Tanzania ikiwa na mtaji wa Dola milioni 425 za Marekani (Sh1.123 trilioni), kati ya hiyo miradi 11 ipo Zanzibar ambayo ina thamani ya Dola milioni 12 (Sh31 bilioni).
“Utaona bado si sehemu kubwa ya kile ambacho tunakitarajia, kwa hiyo tumewaleta hapa ili tuone fursa zaidi na kuwekeza zaidi, Wabelgiji ni wazuri kwenye mifumo na usafirishaji hususani katika bandari, tunachofanya ni kuweka mazingira,” amesema.
Amesema tayari wameingia makubaliano ya ushirikiano kati ya bandari za Tanzania na bandari ya Ubegiji.
Mbali ya hayo, amesema wiki ijayo Tanzania itasaini mkataba na Umoja wa Ulaya wenye thamani ya Euro milioni 15 (Sh41.76 bilioni) ambazo zitasaidia uendeshaji wa bandari zikiwemo za Zanzibar.
“Kwa hiyo ujumbe huu unataka kuleta hayo na yakifanyiwa kazi ajira zinaongezeka, mapato ya Serikali yanaongezeka na ujuzi unaongezeka kwa sababu tutakuwa tunajifunza na kubadilisha teknolojia,” amesema.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi amesema Serikali ya Muungano (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zimejitanaibisha kuweka mazingira bora ya kuvutia wawekezaji na wanashawishika kuja nchini kuwekeza mitaji yao.
Amesema ujio wa kampuni hizo kutoka Ubelgiji na maeneo mengine ni utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi, kuhakikisha wanaitangaza nchi na kuvutia wawekezaji, hivyo inapanua ajira na kuongeza fursa mbalimbali.
“Kwa hiyo ni wajibu wetu na wafanyabiashara hapa nchini tuonyeshe ushirikiano na wawekezaji wanaokuja nchini na kuwa na utayari kama Serikali zote mbili zinavyofanya, kwani wafanyabiashara wanaokuja kuwekeza hapa wanakuwa na nguvu za kiuchumi,” amesema.
Amesema kwa sasa Serikali inaondoa vikwazo na kurekebisha sheria na kanuni zinazosimamia uwekezaji, huku uwapo wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (Zipa) vimesaidia kuondoa urasimu na kurahisisha uwekezaji kwa kufupisha milolongo mirefu.
Waziri Ofisi ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema ujio wa wawekezaji hao umetokana na ziara aliyofanya Rais Samia Suluhu Hassan nchini humo mwaka 2022. Amesema waliyokubaliana ndiyo yamekuja kutekelezwa.
“Watafanya ziara katika maeneo mbalimbali kuona kwa namna gani Zanzibar ina uwezo wa kupokea miradi yao na sisi kama Serikali tumeshawapa yale yote ambayo wanahitaji, hususani sheria za ardhi na sheria za uwekezaji,” amesema.
Amesema kwa sasa Zanzibar imefunguka katika eneo la uwekezaji, hivyo imani yao ni kwamba yataleta matunda makubwa katika kisiwa hicho.
Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Pater Huygherbaert amesema ameambatana na kampuni mbalimbali kutoka nchini humo ambazo zimekuwapo nchini kwa takribani siku nne kuzungumza na wafanyabiashara na kuangalia maeneo ya uwekezaji.
Amesema wameambatana na kampuni za masuala ya bahari, usafirishaji, teknolojia na nyingine nyingi.
“Tanzania ni sehemu nzuri kuwekeza na kufanya biashara, ndiyo maana kumekuwapo mwamko mkubwa wa kampuni kutoka Ubegiji kuwekeza nchini kwa sababu ya mazingira. Watatembelea Mangapwani na wana mengi ya kufanya Zanzibar,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Kitaifa ya Wafanyabiashara, Hamad Hamad amesema ujio wa wafanyabishara hao ni fursa ya kubadilishana uwezo kati ya wafanyabisahara wa Zanzibar na Ubegiji na kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili.
“Sisi tutaangalia maeneo gani tunaweza kufanya biashara hususani katika usafirishaji wa mwani, viungo kama karafuu na tunaendelea na mazungumzo wapi tunaweza kufanya biashara kwa pamoja,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa Zipa, Vuai Yahya Rada, amesema iwapo uwekezaji huo utafanikiwa utaongeza uchumi, kukuza ajira na pato la Taifa.
“Kupitia uwekezaji tutafungua fursa nyingi za ajira na tunaweza kuingiza nchini teknolojia. Katika miradi ambayo imeshawekezwa kutoka Ubelgiji mingi ni maeneo ya utalii na fedha. Zaidi ya ajira 200 zimezalishwa kupitia miradi hiyo,” amesema.