Mwenyekiti Chadema Tanga azungumzia makada waaliokamatwa na polisi

Tanga. Makada wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Tanga wameachiwa baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kufanya fujo kwenye vituo vya kupigia kura.

Makada hao walioachiwa ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Yosefa Komba (38) na Devotha Mpari (48). Pia, watu wengine wawili waliokamatwa kwenye tukio hilo, Sikujua Almasi (38) na Mohamed Juma (40), wameachiwa huru.

Nyanda ya Kaskazini inaundwa na mikoa minne ambayo ni Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.

Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 28, 2024, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje amesema viongozi hao wameachiwa na kuambiwa wakihitajika polisi wataitwa tena kwa ajili ya kutoa taarifa zaidi kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Amesema Komba ameachiwa jana Novemba 27, 2024 usiku baada ya kuhojiwa na polisi lakini Mpari ameachiwa asubuhi ya leo Novemba 28, 2024 na wote wapo huru.

Mwenyekiti huyo amesema tuhuma ya viongozi hao ni kuhusu kufanya fujo kwenye vituo vya kupigia kura, lakini walikuwa wanafuatilia kuhusu uwepo wa baadhi ya vituo kukuta kumekiukwa sheria za uchaguzi.

Mwenyekiti Bahweje ameongeza kuwa makosa yaliyotajwa kwa makada wote wawili yanafanana, ila walikuwa wanawajibika kwenye nafasi zao na hatua zaidi kuhusu matukio yaliotokea watachukua kwa wagombea wao kufanyiwa visa mbalimbali.

 “Kesi ilikuwa kuna vituo walikuta kura kabla ya zoezi la kupiga kura kuanza hivyo wakati wa ufuatiliaji matukio hayo kwa nyakati tofauti, lakini Yosefa ameachiwa jana usiku huku mwenzake Devotha akiachiwa leo asubuhi, na wameambiwa wakihitajika wataitwa,” amesema Jonathan.

Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Muheza, Michael Mguli ameomba mamlaka husika zinazosimamia uchaguzi kuangalia maeneo yote ambayo kulitokea dosari na fujo na kusababisha uchaguzi haukufanyika vizuri, itolewe nafasi kwa wagombea sehemu husika urudiwe.

Amesema kufanya hivyo itasaidia kutoa nafasi kwa waanchi kuweza kurudia uchaguzi na kuchagua viongozi ambao wataona wao kuwa wanawafaa, kwani sehemu yoyote yenye fujo wananchi hawawezi kujitokeza na kuwa huru,kwa kuweza kupiga kura wakihofia.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, jana Novemba 27, 2024 liliwakamata watu wanne wakidaiwa kufanya vurugu kwenye vituo vya kupigia kura katika Wilaya ya Pangani na Tanga mjini wakati upigaji kura ukiendelea.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Novemba 27, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema wananchi hao walikamatwa kwa kosa la kuchana nyaraka za Serikali wakati uchaguzi wa serikali za mitaa ukiendelea baada ya kuripotiwa kuchana karatasi za kura kwa makusudi.

Kamanda Mchunguzi alitaja waliokamatwa kwenye tukio hilo kuwa ni Mohamed Juma (40), mkazi wa Mwanzange jijini Tanga na Devotha Mpari (48), mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mivumoni, kwa kosa la kuchana nyaraka za serikali wakati wa uchaguzi huo.

Wengine ni Yosefa Komba (38) na Sikujua Almasi (38), wote ni wakazi wa Genge wilayani Muheza, kwa kosa la kufanya fujo kwenye kituo cha kupigia kura.

Related Posts