Dar es Salaam. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimepewa heshima ya kutajwa kuwa “Shirika la Kuhamasisha Uwekezaji Lililopiga Hatua zaidi Barani Afrika” katika mkutano wa kila mwaka wa uwekezaji (AIM) 2024 unaofanyika Abu Dhabi Falme za Kiarabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TIC leo Mei 8, 2024, tuzo hiyo imepokewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dk Tausi Kida kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Dk Kida amesema imekuja wakati mwafaka na ni tunu kwa Taifa kwa kuwa inaakisi jitihada za Serikali za kuimarisha mazingira ya biashara nchini zinazoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Tuzo hii inaongeza imani kwa wawekezaji na sisi Serikali hasa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji tutaendelea kuvutia uwekezaji ili kuzalisha ajira na kukuza uchumi wa nchi yetu,” amesema Dk Kida.
Katika kinyang’anyilo cha tuzo hiyo, inayotolewa na waandaaji wa Mkutano wa Mwaka wa Uwekezaji (AIM Congress) unaoendelea Abu Dhabi, TIC imezipiku taasisi mbalimbali za uwekezaji za mataifa ya Afrika kwa kuwa na ongezeko chanya katika vigezo vya Usajili wa Miradi, Thamani ya Uwekezajia na Idadi ya ajira zinazotokana na shughuli za Kituo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa ya TIC, kwenye kigezo cha usajili wa miradi, kwa kipindi cha Januari 1, 2023 hadi Desemba 31, 2023, taasisi hiyo iliongeza miradi inayosajiliwa hadi 526 kutoka 293 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 79.5.
“Katika kigezo cha thamani ya uwekezaji, kati ya Januari 1, 2023 na Desemba 31, 2023, thamani ya uwekezaji iliyowezeshwa na TIC iliongezeka kufikia Dola 5,720.36 milioni (Sh14.84 trilioni) kutoka Dola 4,547.70 milioni (Sh11.8 trilioni) zilizorekodiwa kipindi kama hicho 2022, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.8.
“Vile vile, idadi ya ajira zilizoundwa kutokana na shughuli za TIC kati ya Januari 1, 2023 hadi Desemba 31, 2023, zimeongezeka hadi 137,010 kutoka 40,889 zilizorekodiwa kipindi kama hicho mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 235.1,” imesema taarifa hiyo.