MADAKTARI bingwa 20 kutoka hospitali kubwa nchini wamesafiri kwenda nchini Comoro kwaajili ya kuweka kambi ya wiki moja ya uchunguzi na utoaji huduma za kibingwa za magonjwa mbalimbali ikiwemo upasuaji wa moyo, saratani na ubongo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Madaktari hao wanatoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Mifupa (MOI) na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Dodoma.
Akizungumza jana kabla ya madaktari hao kuondoka, Mratibu wa Utalii Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk. Aisha Mahita, alisema Tanzania imekuwa ikipokewa wagonjwa wengi kutoka nchini Comoro ndiyo sababu wameamua kwenda kuweka kambi ya matibabu ili kuona magonjwa gani yanayowasumbua na kuyawekea mkakati.
“Tunakwenda kutangaza utalii tiba serikali yetu imewekeza kiasi kikubwa kwenye sekta ya afya, tuna mambo mengi sana yamefanyika kwa hiyo lazima dunia ijue kwamba kwenye sekta ya matibabu Tanzania iko vizuri na baada ya Comoro tutakwenda nchi zingine,” alisema
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii Tiba, Abdulmalik Mollel, alisema lengo la safari hiyo ni kuwajengea uwezo madaktari wa Comoro na kuangalia fursa za uwekezaji sekta ya afya zilizopo nchini humo.
“Ninafuraha kumwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii Tiba Kitaifa Profesa Mohamed Janabi kwasababu madaktari kutoka hospitali zetu kubwa kwa usaidizi wa Wizara ya Afya na tutaangalia wadau ambao tunaweza kufanya kazi nao na tutaangalia fursa zilizopo kule na kushauriana na mamlaka husika kuona namna ya kuzitumia,” alisema Mollel
Aliwashukuru wakurugenzi wa hospitali zote zilizotoa madaktari bingwa kwenda kutoa huduma nchini Comoro na pia Mkurugenzi wa JKCI, Dk. Peter Kisenge kwani ndiye mratibu mkuu wa safari hiyo.
“Sehemu kubwa ya mafanikio haya ni uratibu wa Dk. Kisenge kwasababu yeye ndiye amewasiliana na wakurugenzi wenzake wa hospitali zilizotoa madaktari bingwa kwa hiyo sisi Kamati ya Utalii Tiba tunamshukuru kwa kazi kubwa ambayo ameifanya,” alisema Mollel
Pia aliushukuru ubalozi wa Tanzania nchini Comoro kwa namna ambavyo umefanyakazi kubwa kwa kushirikiana na Kamati ya utalii tiba kufanikisha safari hiyo.
Daktari bingwa wa moyo kutoka JKCI, Salehe Hamis alisema watafanya matibabu mbalimbali ikiwemo uchunguzi wa saratani, mifupa, ubongo na moyo ili kuendeleza utamaduni wa kutoa matibabu ya afya kwenye nchi jirani.
“Umekuwa utamaduni wa JKCI kutoa huduma za kibingwa kwenye mikoa mbalimbali nchini na sasa tumeanza kwenda nchi za jirani kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika kwenye upande wa teknoljia na vifaa vya kisasa na safari hii tuna wataalamu kutoka hospitali mbalimbali,” alisema Dk. Hamis.
Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kutoka MOI, Zarina Ali alisema watawajengea uwezo madaktari wan chi hiyo ili waweze kutibu magonjwa ya kawaida ya ubongo na mishipa ya fahamu na kwa yale watakayokuwa wanashindwa wanawaleta wagonjwa kwenye taasisi ya MOI.
“Tutatoa huduma za ubongo, mishipa ya fahamu na ubongo kama sehemu ya kuhamasisha utalii tiba nchini Tanzania na tutashirikiana na wataalamu wa tiba mbalimbali kwa wiki nzima tukiwa kule,” alisema
Daktari bingwa wa saratani kutoka Ocean Road, Mark Athumani alisema kambi hiyo ya matibabu ya wiki moja yatasaidia kuongeza uhusiano wan chi hizo mbili.
“Kwenye msafara huu Ocean road imepeleka wataalamu saba wakiwemo madaktari bingwa watano na watalamu wawili wa uchunguzi wa awali wa maradhi ya saratani kwa hiyo kule tutatoa uchunguzi wa uvimbe mbalimbali,” alisema na kuongeza
“Tutatoa matibabu mbalimbali ya kuwakinga wanawake wasipate saratani ya mlango wa kizazi na saratani za matiti, ngozi na tezi dume na tutatoa pia elimu ya namna ya kujikinga na saratani. Serikali yetu imewekeza sana kwenye tiba ya saratani na kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati sisi ndio wenye mashine bora kabisa ya uchunguzi wa saratani,” alisema.