Wenyeviti waomba nyongeza ya posho

Kibaha . Wenyeviti wa serikali za mitaa 73 kutoka Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani, wameomba kuongezwa kwa posho wanayopokea kutoka Sh10,000 hadi Sh50,000.

Wenyeviti hao wameomba Serikali kufanyia tathmini kiwango hicho wanacholipwa sasa kwa kuwa hakiwawezeshi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Wakizungumza na Mwananchi muda mfupi baada ya kuapishwa wenyeviti hao wamesema kuwa, ingawa wanatambua kuwa kazi hiyo ni ya kujitolea, majukumu wanayotekeleza ni makubwa, hasa katika kuwahudumia wananchi.

“Tunashukuru kwa kuaminiwa na hii ni kazi ya kujitolea kutumikia wananchi, lakini ni vema posho ya Sh10,000 kwa mwezi iongezwe, angalau ifike Sh50,000, kwani tunafanya kazi kubwa sana kuhudumia wananchi,” amesema Abuu Matumla.

Kwa upande wake, Emiliani Mtenga amesema kuwa kazi za mwenyekiti wa serikali ya mtaa haina muda maalumu, kwani wakati wowote wako kazini na kila jambo linawaangalia, hivyo ni muhimu wakazingatiwa na kuongezewa posho.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Tangini, Iddi Mfaume amesema kuwa posho iliyotangazwa na Halmashauri ni ndogo ukilinganisha na majukumu wanayotekeleza, na hivyo kuna umuhimu wa kuangalia uwezekano wa nyongeza.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Dk Rogers Shemwelekwa amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na sheria, ili kuepuka kuwa chanzo cha migogoro katika maeneo yao.

“Nawaomba msiende kujihusisha na migogoro ya ardhi katika maeneo yenu, bali mkatende haki katika kutekeleza majukumu yenu ndani ya jamii,” amesema.

Mbunge wa Kibaha Mjini, Selvestry Koka, amewashauri wenyeviti hao kutambua mipaka ya kazi zao na kushirikiana kwa karibu na maofisa watendaji wa mitaa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mussa Ndomba amesema kuwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo ni mwanzo wa mapambano, akisema kuwa uchaguzi Mkuu ujao unapaswa kuendana na utendaji bora wa viongozi hao.

“Tambueni kuwa kushinda kwa nafasi zenu kumetokana na utendaji mzuri wa Serikali, hivyo ili kulinda heshima hiyo, mnapaswa kuwatumikia wananchi vizuri,” amesisitiza.

Related Posts