Uchafuzi utokanao na moto waua watu milioni 1.5 kila mwaka – DW – 29.11.2024

Hayo ni kulingana na matokeo ya utafiti yaliyotangazwa siku ya Alhamisi. Idadi hii ya vifo inatarajiwa kuongezeka katika miaka ijayo kwani mabadiliko ya hali ya hewa yatasababisha kutokea mara kwa mara kwa mioto ya nyika.

Timu ya kimataifa ya watafiti ilichunguza data zlizopo kuhusu mioto ya mazingira, ambayo inajumuisha moto wa nyika unaotokea kwenye mazingira ya asili na moto uliopangwa kama vile uchomaji wa makusudi kwenye mashamba. 

Watafiti hao walisema vifo takriban 450,000 kwa mwaka vinavyotokana na magonjwa ya moyo vilihusishwa na uchafuzi wa hewa unaotokana na moto kati ya mwaka 2000 na 2019.

Vifo vingine 220,000 vilivyotokana na magonjwa ya kupumua vilihusishwa na moshi na chembechembe zilizotolewa angani na moto.

Kutokana na visababishi vyote duniani, jumla ya vifo milioni 1.53 kwa mwaka vilihusishwa na uchafuzi wa hewa unaotokana na moto wa mandhari, kulingana na utafiti huo.

India | Ukungu
Ukungu mzito ukiwa umetanda majira ya asuhubi katika mojawapo ya vijiji nchini India.Picha: Sakib Ali/Hindustan Times/Sipa USA/picture alliance

Zaidi ya asilimia 90 ya vifo hivi vilikuwa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, na karibu asilimia 40 vilitokea katika kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara pekee.

Nchi zilizo na idadi kubwa ya vifo zilikuwa China, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, India, Indonesia, na Nigeria. 

Kiasi kikubwa cha uchomaji haramu wa mashamba kaskazini mwa India kimehusishwa kwa sehemu na moshi wenye sumu ambao hivi karibuni umekuwa ukisababisha mji mkuu New Delhi kushindwa kupumua vizuri.

Soma pia: COP28: Ahadi za kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi hazitekelezwi ipasavyo

“Sijisikii kwenda nje kwani ninahisi kama Delhi imekuwa chumba cha gesi. Hali imezidi kuwa mbaya na hutaki hata kwenda nje,” alisema mkaazi wa New Delhi aliejitambulisha kwa jina moja la Sohan.

“Serikali haina uwezo wa kudhibiti chochote, haifanyi chochote. Unahisi kama tunaishi kwenye chumba cha gesi,” aliongeza Sohan. 

Uchafuzi wa hewa bado ni tatizo kubwa barani Ulaya

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mkaazi mwingine kwa jina la Amit Kumar Singh alisema: Ni vigumu kuishi Delhi sasa. Uchafuzi unasababisha hisia ya mwako machoni na matatizo ya kupumua unapokuwa nje asubuhi na jioni.

Hatua za dharura zahitajika kushughulikia changamoto hiyo

Waandishi wa utafiti huo wa jarida la Lancet walitoa wito wa “hatua za dharura” kushughulikia idadi kubwa ya vifo vinavyosababishwa na moto wa mandhari.

Walisema tofauti kati ya mataifa tajiri na maskini inasisitiza zaidi kile walihokiita “udhalimu wa tabianchi”, ambamo wale waliochangia kidogo katika ongezeko la joto duniani ndio wanaoumia zaidi.

Baadhi ya njia ambazo watu wanaweza kuepuka moshi kutoka kwenye mioto, kama vile kuhama eneo la moto, kutumia vitakasaji hewa na barakoa, au kukaa ndani, hazipatikani kwa watu katika nchi maskini, watafiti walibainisha. 

Pakistan Lahore | Uchafuzi wa hali ya hewa | Wagonjwa wakitibiwa hospitali.
Wagonjwa wakitibiwa katika hospitali mjini Lahore, Pakistan kutokana na uchafuzi wa hewa.Picha: ARIF ALI/AFP

Kwa hiyo, waliitaka jumuiya ya kimataifa kutoa msaada zaidi wa kifedha na kiteknolojia kwa watu katika nchi zilizoathirika zaidi.

Utafiti huo umetolewa wiki moja baada ya mkutano wa Tabianchi wa Umoja wa Mataifa ambapo wajumbe walikubaliana kuongeza ufadhili wa hali ya hewa ambao nchi zinazoendelea ziliukosoa kuwa hautoshi.

Pia ulichapishwa baada ya Ecuador kutangaza hali ya dharura ya kitaifa kutokana na moto wa msitu ulioteketeza zaidi ya hekta 10,000 kusini mwa nchi hiyo. 

Dunia pia imekuwa ikikumbwa na vimbunga, ukame, mafuriko, na matukio mengine ya hali ya hewa kali wakati wa kile kinachotarajiwa kuwa mwaka wenye joto zaidi katika historia iliyorekodiwa.

Related Posts