Mwanza. Hukumu ya kesi ya kulawiti inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu (RC), Dk Yahya Nawanda inatarajiwa kusomwa leo Ijumaa Novemba 29, 2024, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza.
Kesi hiyo ya kulawiti namba 1883/2024, inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Erick Marley.
Mara ya mwisho kuripoti mwenendo wa kesi hiyo ilikuwa Septemba 10, 2024 baada ya kutopata ushirikiano licha ya Marley kuruhusu wajulishwe mwenendo wa kesi bila kuvunja taratibu kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa ni ya nyuma ya kamera.
Siku hiyo shauri hilo lilitakiwa kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mshtakiwa (Dk Nawanda).
Kabla ya ushahidi wa upande wa mshtakiwa kuanza kutolewa, Julai 16, 2024 mbele ya Hakimu Marley, mashahidi wawili wa Jamhuri ambao ni mwanafunzi anayedaiwa kulawitiwa na Dk Nawanda na mama mzazi wa mwanafunzi huyo walifungua ukurasa wa kutoa ushahidi ambapo waliutoa nyuma ya kamera (faragha).
Kesi hiyo iliitwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Julai 9, 2024, mbele ya Hakimu Marley ambapo mshtakiwa alikana shtaka hilo baada ya kusomewa maelezo ya awali (PH) na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Magreth Mwaseba.
Dk Nawanda anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 2, 2024, katika maegesho ya magari yaliyoko eneo la Rock City Mall wilayani Ilemela, Mkoa wa Mwanza kinyume na kifungu namba 154 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16.
Endelea kufuatilia Mwananchi