Pointi sita za kimkakati Simba CAFCC

SIMBA tayari ina pointi tatu ilizopata juzi kwa kuifunga FC Bravos do Maquis ya Angola nyumbani bao 1-0 kupitia Jean Charles Ahoua dakika ya 27, lakini mashabiki na viongozi wa Simba wameiona timu yao ikicheza chini ya kiwango huku Bravos ambao walifika nchini siku moja kabla ya mechi wakionekana kuwa moto hasa kipindi cha pili.

Kucheza chini ya kiwango kwa Simba, kumemfanya kiungo huyo kutosita kutoa majibu huku timu hiyo hivi sasa ikiwa na mkakati wa kusaka pointi zingine sita ili kufikisha tisa ijiwekee nafasi kubwa ya kwenda robo fainali kwani takwimu zinaonyesha timu nyingi zinazofikisha pointi hizo zinatoboa.

“Hatukuwa na mchezo mzuri lakini tumefanikiwa kukusanya pointi tatu ambazo zimetuongezea morali ya kupambana zaidi kwenye mechi zilizobaki.

“Imebaki michezo mitano, kila mchezo kwetu utakuwa ni fainali lengo ni kupambania pointi tatu kwenye kila mchezo ili kufikia malengo ya kucheza fainali msimu huu.

“Tumekuwa tukipambana kwaajili ya mashabiki ambao wamekuwa wakijitoa kwa wingi kuja kutusapoti, bao nililofunga ni zawadi kwao na nawaomba waendelee kutuamini na kutupa ushirikiano kwenye kila mchezo.”

Simba iliyopo Kundi A katika michuano hiyo, mchezo ujao ni ugenini dhidi ya CS Constantine utakaochezwa  Desemba 8, 2024 nchini Algeria.

Baada ya hapo, itarejea nyumbani Desemba 15, 2024 kucheza dhidi ya CS Sfaxien, kisha Januari 5, 2025 itaenda Tunisia kurudiana na CS Sfaxien. Januari 12, 2025 itakuwa Angola kupambana na Bravos do Maquis, itamalizia nyumbani Januari 19, 2025 dhidi ya CS Constantine.

Hata hivyo, ukiangalia namna Simba ilivyoanza harakati zake hatua ya makundi, suala kubwa ni matokeo waliyoyapata japo ni ushindi mdogo lakini ishu ya kucheza vizuri sio kipaumbele sana kwenye mchezo wa mpira wa miguu hasa hatua kama hii japo mashabiki wanapenda kuiona timu yao ikicheza soka safi na kushinda.

Takwimu zinaonyesha kwamba, Simba ndani ya misimu saba mfululizo ikiwa imefuzu makundi ya michuano ya Caf mara sita ikiwemo msimu huu, tano zilizopita imefanya vizuri na kuvuka kwenda robo fainali kimkakati zaidi kuliko kucheza soka safi.

Katika mikakati hiyo ya Simba, msimu mmoja pekee wa 2020–21 ilimaliza kinara wa kundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini misimu mingine ikishika nafasi ya pili huku mechi zake sita za hatua hiyo zikiwa ni za hesabu kali.

Wakati ambao Simba ilimaliza kinara wa kundi katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2021-22, ilifuzu ikiwa na pointi 13, ikiiacha Al Ahly nafasi ya pili na pointi 11, huku AS Vita Club (7) na Al Merrikh (2) zikifuatia nafasi ya tatu na nne.

Katika msimu huo, Simba haikuangusha pointi yoyote uwanja wa nyumbani ikizifunga Al Ahly (1-0), Al Merrikh (3-0) na AS Vita Club (4-1), huku ugenini ikipoteza mchezo mmoja pekee wa mwisho dhidi ya Al Ahly kwa bao 1-0, lakini ikaenda DR Congo kuichapa AS Vita Club (1-0) na ikaambulia pointi moja kwa Al Merrikh pale Sudan matokeo yakiwa 0–0.

Kwa wastani, Simba imekuwa na wakati mzuri hatua ya makundi huku hesabu zake nyingi zikiangukia kwenye kufikisha angalau pointi 9 kwenda juu kwani zinaonekana kuwawabeba.

Ni mara tatu Simba imefuzu robo fainali baada ya kumaliza na pointi tisa katika kundi lake ambapo ilikuwa msimu wa 2018-19, 2022–23 na 2023–24 zote ikiwa ni Ligi ya Mabingwa. Huku 2021–22 ikimaliza na pointi 10 sawa na kinara RS Berkane katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Msimu wa 2018-19 ambao ulionekana kuwa mgumu zaidi kwa Simba, timu hiyo ilipokea vipigo vizito ugenini kwa kufungwa mechi zote tatu huku yenyewe mikakati yao ikiwa ni kushinda nyumbani zote, haikuwa na sare. Ikamaliza na pointi 9 nyuma ya kinara Al Ahly iliyofikisha 10.

Al Ahly na AS Vita, waliichapa Simba 5-0 katika ardhi ya kwao huku JS Saoura nayo ikishinda 2-0. Lakini timu hizo zikapoteza nyumbani kwa Simba. Wakati huo Simba ilikatiwa tamaa lakini ilivuka mtihani mzito uliokuwa mbele yao.

Katika kuonyesha kwamba ili ufanikiwe kwenye michuano hii ya kimataifa soka safi sio kipaumbele sana zaidi ya matokeo mazuri, mabingwa mara nyingi wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ambao wamecheza fainali 17 na kubeba ubingwa mara 12, kwa misimu ya karibuni wamekuwa wakisuasua hatua ya makundi lakini wakivuka hapo, wanauwasha moto hadi ubingwa.

Al Ahly katika mataji yao manne ya mwisho iliyobeba 2019–20, 2020–21 na 2022–23, ilimaliza nafasi ya pili katika kundi lake na kwenda kuwa mabingwa huku 2023-24 pekee ndiyo iliongoza kundi.

Related Posts