Harare. Kukatika umeme kumewaacha na mshangao wabunge wa Zimbabwe wakati Waziri wa Fedha, Mthuli Ncube, akihitimisha hotuba yake ya bajeti jana Alhamisi Novemba 28, 2024.
Viongozi wakuu wa nchi wakiwemo Rais Emerson Mnangagwa na Makamu wa Rais, Constantino Chiwenga walijikuta wakiwa gizani baada ya umeme huo kukatika.
Kukatika umeme nchini Zimbabwe, takribani saa 12 kila siku, inaelezwa kunachangiwa na ukame wa muda mrefu ambao unaathiri uzalishaji katika Bwawa la Kariba ambalo ndio chanzo kikuu cha umeme nchini humo.
Taa zilipozima, wabunge wa upinzani walipiga kelele kwamba kukatika huko ni kielelezo cha hali halisi ya adha ya umeme nchini humo.
Msemaji wa Mamlaka ya Ugavi wa Umeme ya Zimbabwe (Zesa), George Manyaya ameambia tovuti ya habari ya Zim Live kwamba kukatika kwa umeme hakujapangwa bali kulitokea kwa sababu ya radi.
Endelea kufuatilia Mwananchi.