Shirika la ufuatiliaji wa haki za binadamu nchini Syria, limesema idadi ya vifo katika mapigano yanayoendelea imefikia watu 182, wakiwemo wapiganaji 102 wa kundi la Tahrir-al-Sham, HTS, 19 kutoka makundi washirika na 61 kutoka vikosi vya utawala na makundi yanayoviunga mkono, huku mashambulizi ya ndege za Urusi yakiripotiwa kuua raia 19 katika maeneo ya vijiji vya Aleppo.
HTS na makundi washirika, yakiwemo yale yanayoungwa mkono na nchi jirani ya Uturuki, walikata barabara ya kimataifa ya Damascus-Aleppo inayojulikana kama M5, na kudhibiti makutano ya barabara za M4 na M5, yanayounganisha mji mkuu na ngome ya serikali ya pwani ya Latakia na mji wa pili kwa ukubwa, wa Aleppo.
Soma pia: Israel yafanya mashambulizi katika wilaya moja mjini Damascus
Shambulio hilo linafanyika baada ya wiki kadhaa za vurugu katika eneo hilo, ambapo wanaharakati walisema vikosi vya serikali na washirika wao Urusi vimeongeza mashambulizi katika maeneo ya ngome ya mwisho ya upinzani. Kamanda wa Kijeshi wa Tahiri-al-Sham, Abu Zubair al-Shami, alisema operesheni yao itawaruhusu maelfu ya watu walioyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya serikali katika wiki za hivi karibuni kurejea.
”Baada ya kuanza operesheni ya Vita vya Kuzuia Uvamizi, uvamizi ulilenga watu wetu katika maeneo yaliyokombolewa, ukiongeza mateso yao. Sisi tunachukua jukumu la kusimamisha dhuluma za utawala na kulinda watu wetu. Ukatili ambao adui yetu ameona kutoka kwa wapiganaji wetu ni mwanzo tu.”
Mchambuzi Nick Heras kutoka taasisi ya mikakati na sera ya New Lines, amesema waasi wanajaribu kuzuia uwezekano wa kampeni ya kijeshi ya Syria mkoani Aleppo, ambayo mashambulizi ya anga ya Urusi na serikali ya Syria dhidi ya maeneo ya waasi yamekuwa yakiandaa. Assad: Juhudi za kurejesha uhusiano na Uturuki hazijafanikiwa
Baadhi ya makundi yanayoungwa mkono na Uturuki yameshiriki katika shambulio hilo, na Heras amesema, “Ankara inatoa ujumbe kwa Damascus na Moscow kuacha juhudi zao za kijeshi kaskazini magharibi mwa Syria, na kuongeza kuwa hatua ya Uturuki inaonesha azma ya kuzuia shinikizo la kijeshi la serikali za Syria na Urusi.
Pamoja na Urusi, Rais wa Syria Bashar al-Assad ameungwa mkono katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na Iran na makundi washirika ya wanamgambo, likiwemo la Hezbollah la nchini Lebanon. Shirika la habari la Iran limeripoti kuwa Jenerali wa Kikosi cha Ulinzi wa Mapinduzi ya Iran aliuawa katika mapigano ya Alhamisi.
Soma: Israel yashambulia barabara kuu ya Syria -Lebanon
Heras amesema vikosi vya waasi viko katika nafasi nzuri zaidi ya kuchukua na kushikilia vijiji kuliko vikosi vya serikali ya Syria vinavyoungwa mkono na Urusi, mnamo wakati Wairani wakishughulishwa na hali nchini Lebanon.