Majaji na Mahakimu wa EAC kukutana Jijini Arusha Disemba 2-7.

 Na Jane Edward, Arusha

 Mkutano Mkuu wa 21 wa chama cha majaji na mahakimu wa Afrika Mashariki (EAMJA) unatarajiwa kufanyika jijini Arusha  kuanzia tarehe 2-7 mwezi Disemba mwaka huu.

Akitoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha katika Ofisi za kituo cha utoaji haki Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji wa Mahakama ya rufani na Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi Dkt. Gerald Ndika amesema Rais anatarajiwa kufungua mkutano huo siku ya Jumanne Disemba 3, 2024.

Jaji Dkt Ndika amesema baadhi ya malengo ya Mkutano huo ni kuwapa jukwaa majaji na mahakimu katika ukanda wa Afrika Mashariki kuweza kukutana na kujadili namna bora ya kuboresha utendaji kazi wao, kujadili changamoto, mafanikio pamoja na kupeana uzoefu.

“Malengo mengine ya mkutano huu ni pamoja na kutetea na kulinda uhuru wa mahakama zetu za ukanda wa Afrika Mashariki, kuhakikisha zinakuwa na utawala bora wa sheria kwa sababu nchi yoyote haiwezi kuwa na maendeleo ikiwa ina changamoto ya utawala wa sheria pamoja na mfumo wa utoaji haki” amesema Jaji Dkt. Ndika na kuongeza,

“Kwenye upande wa maudhui ya mkutano huo tutaangalia suala la uboreshaji wa mifumo ya utoaji haki kwa ajili ya kuimarisha utangamano wa ukuazaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki “

Aidha Jaji Dkt. Ndika ametaja maeneo matano mahsusi ambayo yatajadiliwa kwa kina ambayo ni programu za maboresho za mifumo ya utoaji wa haki jinai, programu za maboresho za mifumo wa utoaji haki katika mashauri ya madai kama vile mashauri ya ardhi, mirathi, mikataba pamoja na ajira.

Maeneo mengine ni uboreshaji wa utoaji haki katika migogoro ya kazi ambapo nia ni kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuongeza imani kwa wawekezaji, matumizi ya teknolojia na mawasiliano ili kuongeza ufanisi wa utoaji haki pamoja na uimarishaji wa utoaji wa maamuzi kuhusiana na mashauri ya makosa ya jinai na uhamishaji wa fedha unaovuka mipaka ya nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

“Hizi nchi zetu zimetengenishwa na mipaka lakini kwa bahati mbaya kuna baadhi ya makosa ya jinai ambayo hayatambui hiyo mipaka, hivyo ni muhimu kwa nchi zetu kuangalia maeneo kama haya ili kujua changamoto zilizopo lakini pia kuona namna bora ya kuyakabili” amesema Jaji Dkt. Ndika

Jumla ya wajumbe 392 kutoka nchi za Tanzania Bara, Zanzibar, Kenya, Uganda, Burudi, Rwanda na Sudan Kusini wanatarajia kushiriki mkutano huo huku nchi za DRC na Somalia wakishindwa kuhudhuria kutokana na sababu ambazo zisizojulikana.

Related Posts