Tangazo hilo la serikali ya Chad limetolewa saa chache tu baada ya ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrot nchini humo. Taarifa ya waziri wa Mambo ya nje wa Chad, Abderaman Koulamallah imesema serikali yake imesitisha mkataba wa ushirikiano wa ulinzi uliotiwa saini na Ufaransa. Koullamalah amesema Chad inataka mabadiliko, lakini Ufaransa inasalia kuwa mshirika muhimu.
Wengi wamepokea kwa msangao hatua hiyo ya Chad. ambayo imekuja saa chache baada ya ziara ya waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa. Wakati wa ziara yake mjini Ndjamena, Jean-Nöel Barrot hakuzungumzia suala hilo. Wakati wa tamko la pamoja mwishoni mwa ziara yake, mwenzake wa Chad Abderaman Koulamallah alisema tu kwamba “Ufaransa lazima sasa ifikirie kuwa Chad imekua na imepevuka”.
Kusitishwa kwa ushirikano wa ulinzi kunaamanisha kwamba zaidi ya wanajeshi elfu mmoja wa Ufaransa waliko Chad wanatakiwa kuondoka. Lakini hatua hiyo itafuatia masharti na ndani ya muda uliowekwa katika makubaliano ya ulinzi. Toka uhuru wake Chad imepewa usaidizi wa kijeshi na Ufaransa ambayo ina ngome yake nchini humo.
“Mamlaka za Ufaransa lazima pia zifikirie kuondoa uwepo wao”
Wakati huohuo, Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye ametangaza azma yake yakuondoa wanajeshi wa Ufaransa walioko nchini mwake. Kwenye mahojiano na vyombo vya habari vya Ufaransa likiwemo gazeti maarufu Le Monde, Rais Faye amesema Senegal ni nchi huru, na uhuru wake haukubali uwepo wa kambi za kijeshi za nchi za nje.
“Katika miaka 65 baada ya uhuru wetu, mamlaka za Ufaransa lazima pia zifikirie kuwa na ushirikiano wa kuondoa uwepo wao wa kijeshi. na badala yake kuwepo na ushirikiano ambao ni mzuri, wenye manufaa, unaozingatia pande zote na ushirikiano wenye hadhi ya kimataifa kama tulio nao na nchi nyingine nyingi.”, alisema Diamoye Faye.
Kauli hii ya rais wa Senegal imekuja baada ya mazungumzo yake wiki iliopita na Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye alimuakika kufanya ziara mjini Moscow Januari mwakani.
Hatua ya Chad na Senegal ya kutaka kuondoka kwa wanajeshi wa Ufaransa ni pigo jipya kwa diplomasia ya rais Macron, ambayo imeshuhudia jeshi lake likifukuzwa kutoka Mali, Niger na Burkina Faso katika miaka ya hivi karibuni.
Hadi sasa Uafaransa inawanajeshi mia saba nchini Senegal na Gabon, mia sita nchini Cote d’Ivoire na zaidi ya elfu moja huko Chad.