Dar es Salaam. Maisha lazima yaendelee. Ni kauli za wafanyabiashara kwenye maghorofa mawili yaliyo pembeni ya lile lililoporomoka katika soko la Kariakoo ambao sasa wanaendelea na shughuli zao za kibiashara.
Majengo hayo mawili yalitakiwa kuchunguzwa usalama wake, mara baada ya ajali ya kuporomoka kwa jengo jirani na kusababisha vifo vya watu 29, majeruhi 88 na hasara ya mali.
Jengo la upande wa kulia katika harakati za uokoaji ndilo lilitobolewa matundu chini, yaliyotumiwa na waokoaji.
Lile lililopo upande wa kushoto nalo lilichimbwa pembezoni na kusababisha msingi wake kuwa wazi, jambo ambalo lilizua hufu kuwa huenda nayo si salama.
Baada ya shughuli ya uokozi kukamilika hivi karibuni, Msemaji wa Serikali, Thobias Makoba alisema maduka ya majengo hayo mawili hayatafunguliwa hadi timu ya wataalamu itakapojiridhisha usalama wake.
Mwananchi leo Novemba 29 imeshuhudia shughuli mbalimbali zikiendelea katika majengo hayo na maduka yakiwa wamefunguliwa kwenye jengo lililo upande wa kulia wa lile lililoporomoka.
Baadhi ya wafanyabiashara ambao hawakutaka kutaja majina yao wamesema, mwanzo walikuwa na hofu, lakini sasa wapo sawa na wanaendelea na biashara kama kawaida.
“Maisha lazima yaendelee, ili jengo tunaamini ni imara na kama unavyotuona tunaendelea na kazi,” alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko hilo, Martine Mbwana amesema hao wanatoa tu mizigo yao si kufanya biashara.
Mbali na maduka kufunguliwa, pia nje ya jengo hilo kulikuwa na biashara zikiendelea, huku msongamano wa watu kwenye mtaa ukirudi kama awali.
Kwenye jengo la upande wa kushoto, baadhi ya watu walikuwa juu wakihamisha mizigo yao kwenda eneo tofauti.
Mmoja wa wafanyabiashara kwenye jengo hilo alisema wanahama kwa kuhofia usalama wa jengo hilo.
“Kazi inaendelea juu na wengine wapo chini wanahamisha mizigo yao, kila mmoja anapeleka anapopajua,” alisema mfanyabiashara mwingine
Inaelezwa kuwa mizigo iliyo ndani ya jengo hilo inahamishwa kwa njia mbadala kutokana ile waliyokuwa wakiitumia kuharibika kwenye jengo jirani kuporomoka.
“Tulikuwa tukitumia njia ambayo ilikuwa kwenye jengo lililoporomoka, hivyo ili kuhamisha mizigo yetu, tumetoboa jengo ili kwa nyuma na kuitolea huko,” alisema.