Unguja. Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), amewataka watendaji wakuu wa Serikali kuwa makini na utunzaji wa taarifa binafsi kwani kwenye taasisi kuna nyaraka nyingi za siri za watu, hivyo bila ulinzi inaweza kusababisha madhara makubwa kwa wananchi iwapo zikitumika vibaya.
Zena ametoa kauli hiyo leo Novemba 29, 2024 wakati wa semina kwa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa SMZ iliyoandaliwa na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC).
“Madhara ni makubwa iwapo taarifa binafsi zikitumika ndivyo sivyo, maendeleo ya teknolojia yanaleta tishio katika taarifa binafsi, matishio ni makubwa yanaletwa katika njia ya ushawishi wakati mwingine huwezi kushuku, watu wamekuwa wakiombwa fedha kwa utapeli lakini hayo yote ni baada ya kuwa wamepata taarifa binafsi za watu,” amesema.
Sheria namba 11 ya Taarifa Binafsi ilitungwa mwaka 2022, na PDPC ikaundwa mwaka 2023 kabla ya kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Mei, 2023.
Amesema kwa sasa Zanzibar inaandaa sheria ya kulinda masuala binafsi ili kuweka mfanano na ile ya Tanzania Bara.
Mkurugenzi wa PDPC, Emmanuel Lameck amesema ulinzi wa taarifa binafsi ni haki ya msingi ya binadamu na kupitia katiba zote mbili ya Tanzania na ya Zanzibar kupitia ibara ya 16 na 15 zimetaja kuwa na ulinzi wa taarifa.
“Hizi taarifa binafsi ndiyo zinazomwakilisha mtu katika maisha tunayoongelea kwa sasa, dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi si tu ni muhimu wakati huu, bali pia ni muhimu katika ulimwengu wa mabadiliko makubwa ya kidijitali duniani yanayokua kwa kasi.
“Ni wajibu kama viongozi na watumishi wa umma kuhakikisha haki hii inaheshimiwa katika mamlaka zetu, Serikali imefanya jitihada binafsi kutambua umuhimu wa faragha za watu lakini taknolojia inaendelea kukua na kuleta fursa na changamoto mbalimbali,” amesema.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kadri teknoljia inavyoendelea kukua ndivyo inavyooneka kuwa na changamoto ya taarifa binafsi kwa hiyo ipo haja ya kuwa na sheria kwa ajili ya ulinzi wa taarifa na kulinda utu.
Amesema semina hiyo si tu kujadili mfumo wa sheria bali pia hatua zinazoweza kuchukuliwa kutekeleza sheria na kuhakikisha uwajibikaji unakuwapo, kwa hiyo kwa pamoja wanaweza kulinda raia na kukuza imani ya umma katika taasisi, hususani za Serikali.
Amesema ulinzi wa taarifa binafsi si tu ni hitaji la kisheria bali ni kipengele muhimu cha utawala bora na kukuza uwazi, uwajibikaji na heshima kwa haki za raia.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tume hiyo, Adadi Rajab amesema mafunzo hayo yatawasaidia kutengeneza sheria kwa ajili ya kulinda taarifa zao.
Amesema makatibu wakuu ndio wanaofanya kazi nyingi na wanaotengeneza sera na miswada kwa hiyo ndio wa kutafsiri.
“Tunajua mpo kwenye mchakato wa kutengeneza sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi, sisi Bara tumeshatengeneza lakini tumechelewa kwa hiyo kama nanyi mmeanza mchakato ili tuwe na sheria moja ambayo inaeleweka, kwani ilikuwa inatumika kwenye wizara ambazo ni za Muungano tu,” amesema.