Huko Championship vita inaendelea | Mwanaspoti

KIVUMBI cha Ligi ya Championship kinaendelea kurindima ambapo baada ya leo kuchezwa michezo mitatu kesho mingine mitatu pia itapigwa katika viwanja mbalimbali, huku kila timu ikisaka pointi tatu ili kujiwekea mazingira mazuri huko mbeleni.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana utapigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu Geita ambapo wenyeji Geita Gold iliyoichapa mabao 2-1, Cosmopolitan mechi iliyopita itacheza dhidi ya Green Warriors iliyonyukwa na Maafande wenzao wa Polisi Tanzania 2-0.

Saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha wenyeji Mbuni iliyochapwa mabao 4-1 na African Sports itacheza dhidi ya Mtibwa Sugar yenye kumbukumbu nzuri ya kuifunga TMA uwanjani hapo mechi yake ya mwisho kwa mabao 2-1.

Mchezo wa mwisho kesho utapigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara ambapo Mbeya Kwanza iliyotoka kuifunga Transit Camp mabao 2-1, mechi ya mwisho, itacheza na Kiluvya United ambayo hadi sasa haijashinda katika michezo 10, iliyocheza.

Keshokutwa Jumapili itapigwa michezo miwili ambapo Mbeya City iliyolazimishwa sare ya mabao 3-3, dhidi ya Stand United mechi ya mwisho itaikaribisha Biashara United kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya ambayo ilitoka sare pia ya 1-1 na Songea United.

Raundi ya 11 ya Ligi hiyo itahitimisha wikiendi kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga ambapo ‘Chama la Wana’ Stand United iliyotoka sare ya mabao 3-3 na Mbeya City, itacheza na Songea United iliyofungana kwa bao 1-1, dhidi ya Biashara United.

Kocha wa Polisi Tanzania, Bernard Fabian alisema kadri Ligi hiyo inavyozidi kusonga mbele ushindani unaongezeka, ingawa hadi sasa hakuna mwenye uhakika wa kupanda daraja kutokana na kutopishana kwa pointi kati ya timu za juu na za chini.

“Ukiangalia timu zilizopo juu na zile za chini utaona hakuna tofauti kubwa sana, ni mapema kusema kuna mwenye uhakika wa kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, ndio maana kila mchezo unauona ni mgumu bila ya kujali unacheza nyumbani au ugenini.”

Related Posts