Upatikanaji fedha kikwazo utekelezaji mtalaa mpya

Unguja. Kukosekana fedha imeelezwa kuwa miongoni mwa changamoto ya utekelezaji kwa vitendo mtalaa mpya na uandaaji wa umahiri wa wanafunzi Zanzibar.

Hali hiyo imesababisha vitabu kuchelewa kupatikana hivyo kusababisha kudorora kwa huduma za mafunzo.

Hayo yameelezwa leo Novemba 29, 2024 na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdugulam Hussein wakati wa mkutano wa 17 wa Baraza la Wawakilishi.

Alikuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir ambaye alitaka kujua ni aina gani za umahiri zinatarajiwa kutengeneza kwa wanfunzi na changamoto zipi wizara inazipitia katika kuutekeleza kwa vitendo mtalaa mpya.

“Changamoto iliyopo katika utekelezaji kwa vitendo mtalaa mpya ni kutopatikana fedha kwa wakati kunakopelekea kuchelewa kwa upatikanaji wa vitabu pamoja na kudorora kwa huduma za mafunzo,” amesema.

Akizungumza kuhusu aina za umahiri zinazotokana na mtalaa mpya amesema ni utendaji wa matendo mbalimbali ya ubunifu na ujasiriamali kuanzia ngazi ya elimu ya maandalizi, msingi hadi sekondari.

Pia kumjenga mwanafunzi kupata stadi za karne ya 21 ikiwemo kuwa mdadisi, kufikiri kwa kina, kushirikiana na kutatua matatizo, kumfanya mwanafunzi aweze kutenda vitendo mbalimbali vikiwemo ubunifu, uchoraji, uundaji, michezo, ususi, uimbaji na upambaji.

Kwa upande wa elimu ya sekondari, amesema kuna somo la lazima la elimu ya biashara ambalo mwanafunzi ataweza kupata maarifa ya kujua namna ya kujihusisha na kutekeleza shughuli za kibiashara akiwa bado yupo katika elimu ya lazima.

Katika hatua nyingine, amesema wizara imewapima watoto zaidi ya 2000, Unguja na Pemba na matokeo yameonyesha asilimia 85 ya watoto wa maandalizi wameweza kusoma, kuhesabu na kuandika.

Hata hivyo, amesema kwa kuwa bado wapo mwanzoni mwa utekelezaji wa mtalaa mpya wa ngazi ya maandalizi, changamoto kubwa iliyokuwa iliyokuwapo ni uchache wa walimu wa maandalizi, wingi wa wanafunzi katika darasa kwa baadhi ya maeneo na uchache wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

“Kwa sasa wizara imegawa vitabu kwa shule zote za maandalizi kwa mwaka wa kwanza na ipo katika hatua ya uandaaji wa vitabu vya mwaka wa pili,” amesema.

Amesema wizara inaendelea kuimarisha elimu ya awali katika shule zote za maandalizi kwa kuajiri walimu zaidi wa maandalizi, kujenga shule mpya za maandalizi kwa kila wilaya shule mbili.

Related Posts