BAADA ya safu yake ya ulinzi na ushambuliaji kushindwa kuendana na kasi, kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata ameuomba uongozi kusajili maeneo hayo.
Dirisha dogo la usajili linatarajia kufunguliwa Desema 15 mwaka huu, safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwenye mechi 11 walizocheza imefunga mabao matano huku ukuta ukiruhusu mabao tisa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makata alisema timu yake inaangushwa na safu butu na ulinzi mbovu kutokana na baadhi ya wachezaji wanaocheza nafasi hizo kupata majeraha.
“Mfano eneo la ushambuliaji tunae Samson Mbangula ambaye ni majeruhi na eneo la ulinzi Nurdin Chona pia yupo nje ya uwanja anajiuguza nafasi zao zimezibwa na vijana ambao wanachipukia,” alisema.
“Kukosekana kwao wakiwa na uzoefu mkubwa kumeleta changamoto ukuta umekuwa ukiruhusu mabao dakika za mapema sana mechi tatu mfululizo hiyo changamoto imetokea na tukifungwa hatuwezi kurudisha.”
Makata alisema kutokana na changamoto hiyo ameuomba uongozi kumuongezea wachezaji wazoefu kwenye nafasi hizo mbili ili kuongeza changamoto ya ushindani.
“Wachezaji waliopi kwenye safu ya ushambuliaji wanauwezo wa kutengeneza nafasi lakini wanashindwa kuzitumi nitafanyia kazi hiyo kabla ya kuongeza nguvu ili kuweka uwiano mzuri wa kufunga mabao na kupunguza makosa eneo la ulinzi.”
Tanzania Prisons ipo nafasi ya 12 imecheza mechi 11 ikishinda mbili, sare nne na kupoteza michezo mitano imefanikiwa kukusanya pointi 10.