Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu watatu, akiwemo aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti kwa tiketi ya Chadema, Mtaa wa Buswelu A wilayani Ilemela, Pastory Apolinary, kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa, wakati alijificha ili kukwepa kuendelea kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Ijumaa Novemba 29, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema uchunguzi wa polisi ulibaini kuwa Pastory hakutekwa bali alijificha.
Kamanda Mutafungwa amefafanua kuwa taarifa za kutekwa kwa Pastory zilitolewa kupitia Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje, aliyedai kuwa mgombea huyo alitekwa Novemba 25, 2024, saa 7 mchana, baada ya kukamilisha maandalizi ya mkutano wake wa hadhara.
“Baada ya taarifa hizo kusambazwa, Jeshi la Polisi lilifungua jarada la uchunguzi katika Kituo cha Polisi Buswelu saa 11:00 jioni, siku hiyo hiyo, na kuanza kufuatilia suala hilo kwa kina,” amesema Kamanda Mutafungwa.
Amesema uchunguzi ulionyesha kuwa Pastory alituma ujumbe wa uongo kwa kutumia laini zake za simu akidai kuwa alitekwa na watu wasiojulikana, ambao walimfunga kitambaa cheusi usoni.
Hata hivyo, baada ya kuhoji watu mbalimbali, ikiwemo mke wake Maria Mchonyo na Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Buswelu A, Godson Mkama, walibaini taarifa hizo hazikuwa na ukweli.
“Ofisa Mtendaji wa Mtaa alieleza kuwa Novemba 25, 2024, saa 5 asubuhi, alikutana na Pastory ambaye alikiri kuwa hakuwa tayari kuendelea kugombea nafasi ya uenyekiti kwa sababu zake binafsi. Alisema pia kuwa ataondoka eneo hilo hadi uchaguzi utakapoisha,” amesema Kamanda Mutafungwa.
Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata Pastory usiku wa kuamkia leo, akiwa amejificha kwa ndugu yake, Zaituni Misonge, katika Mtaa wa Bugila A wilayani Ilemela.
“Baada ya kukamatwa, Pastory alikiri kuwa hakutekwa bali aliamua kuachana na mchakato wa uchaguzi kwa sababu zake binafsi,” amesema Kamanda huyo.
Pia, Zaituni Misonge (34) na Aneth Bumali (20) wamekamatwa kwa kosa la kumficha Pastory huku wakijua taarifa za kutekwa kwake si za kweli.
“Watu hao wanahojiwa na polisi, na baada ya uchunguzi kukamilika, jalada litapelekwa Ofisi ya Mashtaka ya Mkoa kwa ajili ya hatua za kisheria,” amesema Kamanda Mutafungwa.