RC achekelea Yanga, Singida BS kutimua makocha

MKUU wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amesema amefurahishwa na kiwango kinachoonyeshwa na timu ya Tabora United  kwenye Ligi kuu Bara ambapo imezifunga Yanga mabao 3-1 na kutoka sare ya 2-2 na Singida Big Stars ambzo zote  zimefukuza makocha.

Akizungumza na Mwanaspoti, leo Novemba 29,2024,  Chacha amesema Tabora United itaendelea kuwa bora kwani inapata mahitaji yote muhimu kwa wakati, hivyo kazi kwa sasa ni kucheza soka jambo ambalo ndio siri ya timu hiyo kufanya vyema.

“Nafurahishwa sana na kiwango kinachoonyeshwa na timu yetu na tuliwaambia kwamba matatizo madogo madogo tutayafanyia kazi ili wacheze mpira, maana tunawalipa vizuri, tumewanunulia gari zuri wanasafiri kwa raha kwa hiyo hatutegemei kuona matokeo mabaya, hivyo naridhishwa na mwenendo wa timu yetu,” amesema.

“Tumewafunga Yanga wamefukuza kocha na sasa tumetoka sare na wale Singida Big Stars tena ilikuwa bahati wamecheza asubuhi na wao wamefukuza makocha, hiki ndicho tunakitaka maana tunataka furaha zaidi kwenye mkoa wetu na tunajivunia timu bora.”

Kutokana na timu hiyo kuwa na kiwango bora mkuu huyo wa mkoa amewatahadharisha viongozi kujiepusha na vitendo vya kupanga matokeo kwa ajili ya kuihujumu kutokana na kiwango inachoonyesha na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Timu hii inaangaliwa na wana Tabora. Hiivi tunavyofanya vizuri kwenye Ligi kuu wengi hawapendi hata kidogo. Wako ambao wanaweza kuwaza kupokea pesa ili timu yetu ifungwe sasa kwa atakayebainika nimeshamwagiza kamanda wa polisi wa mkoa akamatwe aende mahabusu moja kwa moja.

“Kwa hivyo viongozi wa timu wasijekufanya makosa kwenye hili,” amesema Chacha

Tabora United leo imecheza mchezo wa Ligi kuu na kuibuka na ushindi wa bao 2-0 dhidi ya KMC kwenye uwanja wa KMC Comolex ambapo timu hiyo imeendelea kujikita nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi baada ya michezo 13 na kufanikiwa kukusanya alama 21, huku KMC wao wakiwa nafasi ya 10 na michezo 13 wakiwa na alama 14.

Related Posts