Samia ataja mikakati Tanzania kupata nishati safi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja mikakati ya kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na nishati safi kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa pamoja na kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na umeme.

Ameyasema hayo leo Novemba 29, 2024 alipokuwa akishiriki mjadala wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha, ikiwa ni maadhimisho ya safari ya miaka 25 ya kuundwa kwa jumuiya hiyo.

Akijibu swali la Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva aliyemuuliza siri ya mafanikio ya nishati safi na utunzaji wa mazingira, Rais Samia amesema licha ya gharama kubwa za upatikanaji wa nishati safi, Tanzania imeweka mikakati vyanzo vya nishati hiyo.

“Kwanza tumechukua jitihada ya kusambaza umeme karibu nchi nzima. Nchi yetu ina vijiji 12,300 na karibu vijiji vyote vimepata umeme, kazi tunayofanya sasa ni kuwaunganisha, kwa sababu umeme kuingia kwenye kijiji haina maana kila mtu amepata,” amesema.

Amesema upatikanaji wa umeme vijijini unawasaidia wanawake kutumia nishati chafu, huku vijana wakiutumia kujiajiri.

“Sasa hivi wimbi la vijana kutoka vijijini kuja mijini limepungua, kwa sababu walichokuwa wanakifuata mijini wanakipata,” amesema.

Amesema miongoni vyanzo vya nishati hiyo ni gesi inayozalisha nusu ya umeme nchini.

“Halafu kuna maji, tuna mabwawa kadhaa yanayozalisha umeme, tuna bwawa kubwa la Nyerere (JNHPP) linalotoa megawati nyingi kama 2,115 na tuna mabwawa madogo,” amesema, akitaja pia uzalishaji wa ueme wa jua na upepo.  

Rais Samia amesema licha ya kuwepo kwa msukumo duniani kote wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, gharama za kuipata ni kubwa, huku mataifa yanayoongoza kwa uchafuzi wa mazingira yakishindwa kuchangia gharama za udhibiti wa hewa chafu.

“Masuala haya ya mabadiliko ya tabia nchi yana gharama kubwa kwa nchi zetu, kwa mfano Tanzania tunatumia asilimia nne mpaka tano ya GDP (pato la ndani la Taifa) yetu kwenye mapambamno ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi,” amesema.

Amesema licha ya kuwepo kwa jitihada za ulinzi wa mazingira, lakini hazifiki matarajio.

“Tanzania pekee tunahitaji Dola 19 bilioni (zaidi ya Sh50 trilioni) katika kipindi cha miaka mitano kutoka mwaka tulionao hadi 2030 kurekebisha hayo mambo ya mazingira, lakini tunakwenda ma-COP na ma-COP, 29, 30, 27 hakuna pesa inatoka  ikitoka ni ndogo na inapotoka haikidhi haja ya kutatua yale  matatizo tuliyonayo,” amesema.

Kwa upande wake,  Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema licha ya kuundwa kwa jumuiya hiyo, eneo la Afrika Mashariki limekuwa na muungano wa biashara kwa zaidi ya miaka 1,000.

“Kuna eneo la Afrika Mashariki (pwani), nyika ya Tanzania katikati na maziwa makuu. Haya maeneo yalikuwa yameunganishwa kibiashara kwa zaidi ya miaka 1,000,” amesema.

Ametoa mfano wa uzalishaji wa mpunga, akisema haiwezekani kufungiana mipaka ya kibiashara.

“Baadhi ya Waganda walinitaka nipige marufuku mpunga kutoka Tanzania, wakasema unaua mpunga wa Uganda.

“Sikukubali kwa sababu kuna makosa manne, kwanza nawalazimisha Waganda kununua mpunga wa bei ghali kutoka kwa wazalishaji wasio na ufanisi, pili ninawakandamiza wazalishaji wa mpunga wa Tanzania, tatu nawadumaza wakulima wa Uganda na nne kama nitapiga marufuku nao watalipiza kisasi, siwezi kufanya hiyo kazi.

“Mpunga ni chakula cha Wahindi na Wachina na watu wengine, kama huwezi, lima muhogo,” amesema.  

Viongozi wengine waliohudhuria mdahalo huo ni pamoja na Rais wa Sudan Kusini Salvaa Kiir, Rais wa Kenya William Ruto, Makamu wa Rais wa Burundi Prosper Bazombanza na Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud.

Related Posts