Dar es Salaam. Mahakama ya Juu ya Ontario, Canada imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa na wakazi wa Tanzania waliokuwa wakilalamikia ukiukwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na Jeshi la Polisi Tanzania karibu na mgodi wa North Mara.
Katika uamuzi huo wa Novemba 28, 2024 Mahakama hiyo imeamua kuwa Ontario si jukwaa mwafaka la kusikiliza madai hayo. Hii ni hatua muhimu kwa Barrick, ambayo imekuwa ikikana mara kwa mara madai hayo, ikiyataja kama yasiyo na msingi na yaliyosambazwa na mashirika fulani yasiyo ya kiserikali.
Barrick ndiyo mmiliki mkuu wa kampuni ya madini ya Twiga Minerals ambayo ni ubia kati ya kampuni hiyo na Serikali ya Tanzania ambayo ina milikia asilimia 16. Twiga Minerals ina miliki migodi ya North Mara na Bulyankuru.
Kufuatia uamuzi huo Rais na Mtendaji Mkuu wa Barrick, Mark Bristow, amesema kampuni hiyo imekanusha mara kwa mara kile inachokiona kama madai yasiyo na msingi yanayotolewa asasi chache zisizo za serikali zenye mrengo wa kiwanaharakati zinaodai kuwapo kwa ukiukwaji wa kihistoria wa haki za binadamu katika maeneo yanayozunguka mgodi wake wa North Mara.
“Tunajivunia mafanikio tuliyoyapata nchini Tanzania kutokana na ushirikiano wetu na Serikali ya nchi hiyo kupitia ubia wa Twiga. Mchango wa mapato ya migodi yetu umeleta mageuzi katika uchumi wa nchi hiyo wakati uwekezaji wetu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” amesema.
Bristow amesema kampuni hiyo itaendelea kujivunia ushirikiano wetu na Serikali ya Tanzania kupitia ubia wa Twiga, ambao umetoa mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa na maendeleo ya jamii zinazozunguka migodi yao.
Katika taarifa yake juu ya uamuzi huo ameeleza kuwa, Barrick imewekeza katika miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kwa lengo la kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo yanayozunguka mgodi wa North Mara. Kampuni hiyo pia inasisitiza kuwa madai yoyote ya ukiukwaji wa haki yanapaswa kushughulikiwa ndani ya Tanzania, si katika mahakama za nje.
Itakumbukwa kuwa, kampuni hiyo imekuwa ikikabiliana na kesi mbili tofauti zilizofunguliwa Novemba 2022 katika Mahakama ya Juu ya Ontario, zikihusiana na matukio ya kiusalama yanayodaiwa kutokea karibu na mgodi huo.
Katika hoja zake, Barrick imekuwa ikidai kuwa madai hayo yanapaswa kushughulikiwa na mamlaka husika nchini Tanzania, kwani wahusika wa karibu zaidi ni Kampuni ya North Mara Gold Mine Limited (NMGML) na Jeshi la Polisi Tanzania (TPF).
Kwa uamuzi huu, Barrick imesema itaendelea kuimarisha shughuli zake nchini Tanzania huku ikizingatia viwango vya juu vya uwajibikaji wa kijamii na kiuchumi.