Dk Biteko: Kukosekana kwa fedha ndiyo sababu mipango mingi kutokamilika

Dar es Salaam. Kukosekana kwa fedha kumetajwa kuwa moja ya sababu ya mipango mikakati mingi inayoanzishwa katika ngazi ya kitaifa na kidunia kushindwa kutekelezeka kikamilifu.

Hiyo ni kutokana na baadhi ya fedha kusubiriwa kutoka mataifa mengine jambo ambalo huweka ugumu katika ufikiaji wa malengo kwa asilimia 100.

Hayo yamesemwa leo na Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko wakati akifungua Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Jumuiya ya Mamlaka za Usimamizi wa Usafiri Majini Barani Afrika, unaofanyika kuanzia leo Novemba 29 hadi 01 Desemba Mosi, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini hapa.

Ametoa kauli hiyo ikiwa ni baada ya Katibu Mkuu wa Shirika la Bahari Duniani (IMO), Antonio Dominguez kueleza namna Afrika ilivyo katika nafasi nzuri ya kuanza kuvutia ushirikiano, uwekezaji, na uhusiano wa shughuli zitakazochochea kuondoa uzalishaji wa hewa ya ukaa kutoka sekta ya usafirishaji baharini kutoka pande zote za dunia.

Dominguez Ametoa kauli hiyo baada ya kuainisha mkakati uliopo unataka kuhakikisha kuwa hakuna uzalishaji wa ufikiaji sifuri wa uzalishaji wa hewa ya ukaa mwaka 2050 katika shughuli za usafirishaji majini.

Akizungumza wakati wa kufungua rasmi mkutano huo, Dk Biteko amesema mipango mingi inayohitaji utekelezaji imekuwa ikikwama njiani kutokana na kukosekana kwa fedha.

Amesema alipokuwa kwenye chumba cha kusubiri kabla ya kuingia katika mkutano huo alikaa na Katibu Mkuu wakijadili mchakato wa kupunguza uzalishaji hewa ukaa huku akihoji kwa nini mikakati mingi inayoanzishwa imekuwa haitekelezwi kikamilifu.

Amesema Katibu Mkuu alimjibu kuwa malengo hayo yamekuwa hayafikiwi kwa sababu mbalimbali lakini ya kwanza ni fedha huku akieleza kuwa kama angeuliza sababu ya pili ingekuwa fedha tena.

“Lakini changamoto gani zinazotupeleka nyuma? Kwa sababu kila tunapokutana, tunajadili mada hiyohiyo, tunaweka tarehe ya mwisho, kama vile ifikapo 2030, tutakuwa na uzalishaji sifuri lakini tunapofika 2030, tunaongeza miaka mingine. Hatuchukui hata muda kutafakari kwa nini hatujapata kile tunachohitaji,” amesema Dk Biteko.

“Lakini wanachama wa mkutano huu, lazima tuanze mahali fulani. Ikiwa tutakaa tu na kungojea fedha zitiririke ili tuweze kutekeleza miradi, niamini, miaka mia moja ijayo tutakuwa tunajiwekea malengo ambayo hayawezi kufikiwa. Kwa sababu tunahitaji fedha,” amesema Dk Biteko.

Akizungumzia suala la mabadiliko ya nishati kuelekea hewa safi ili kukomesha uzalishaji hewa ukaa amesema takwimu zinaonyesha kuwa dunia inahitaji zaidi ya dola trilioni 4 kila mwaka ili kufanya kubadilisha matumizi ya nishati ya asilia kwenda kwenye nishati safi.

“Je, tutapata wapi fedha hizi? Nadhani huu ni wakati wa kila nchi kufanya juhudi hata kwa nafasi ndogo wanayoweza, ili tuendelee kusonga mbele. Angalau baada ya miaka kadhaa, tutaweza kufanikisha kufikia ulimwengu wa nishati isiyozalishaji  hewa ukaa,” amesema Dk Biteko.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Dominguez amesema Afrika iko katika nafasi nzuri kuanza kuvutia ushirikiano, uwekezaji na uhusiano na sehemu zote za ulimwengu kwa ajili ya kufanya mageuzi ya nishati kufikia uzalishaji sifuri wa hewa ya ukaa

“Fursa kubwa zilizopo barani Afrika, hususan katika nishati mbadala, zinaweza kutumika kwa ajili ya uzalishaji na usambazaji wa nishati mbadala na mafuta yasiyo na gesi chafu ambayo sekta ya usafirishaji duniani itahitaji,” amesema Dominguez.

Kwa mujibu wake utafiti uliofanywa na Jukwaa la Uchumi Duniani mapema mwaka huu ulionyesha kuwa asilimia 27 ya umeme wote unaohitajika barani Afrika unaweza kutoka katika vyanzo vya nishati mbadala ifikapo mwaka 2040.

“Hili linaiweka Afrika katika nafasi nzuri ya kunufaika na fursa zote ambazo mchakato huu wa mpito wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaleta,” amesema.

Katika hilo, sekta ya nishati inayo nafasi kubwa ya kushiriki katika kutokomeza hewa ukaa katika sekta ya usafirishaji kwani jambo hilo linahitaji jitihada za pamoja.

Amesema ipo mifano na inayoonyesha hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Afrika, kama vile Muungano wa Afrika wa Nishati ya Haidrojeni Kijani (African Green Hydrogen Alliance), ulioanzishwa na nchi sita za pwani ikiwemo Misri, Kenya, Moritania, Morocco, Namibia, na Afrika Kusini.

“Tunapofanikisha hili, tunaboresha uwezo wa kiuchumi wa baharini wa Afrika na nafasi yake katika ulimwengu. Sasa ni wakati wa kuanza kuangalia uwezo wote uliopo, kuanzia teknolojia hadi jukumu la rasilimali watu katika mchakato huu wote. Lakini lazima tuonyeshe dhamira thabiti kutoka kwenu nyote,” amesema.

Related Posts