Vijana wapewa mafunzo namna ya kujiajiri

Dar es Salaam. Katika juhudi za kupambana na uhaba wa ajira nchini, taasisi ya Her Initiative kwa kushirikiana na Sheria Kiganjani wametoa mafunzo maalumu kwa vijana 50 wa Kitanzania kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kujitambua katika soko la ajira.

Mpango huo unalenga kuwafikia zaidi ya vijana 4,000 na kuwapa mwongozo wa namna ya kujiajiri na kuajiriwa ndani na nje ya nchi.

Mafunzo haya, yaliyofanyika leo Novemba 29, 2024, yameendeshwa na Mkurugenzi wa Teknolojia wa Sheria Kiganjani, Mussa Kisena, aliyesisitiza umuhimu wa kuwaonyesha vijana fursa zilizopo katika soko la ajira.

“Mafunzo haya yanasaidia vijana kutambua nafasi zilizopo kwenye soko la ajira na namna ya kujiandaa ipasavyo. Vijana wengi hawajui jinsi ya kuomba kazi, hivyo tumewapa mbinu za kuandika barua za kazi na kujiandaa kwa mahojiano,” amesema Kisena.

Kisena ameongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia vijana hao kujipanga vizuri ili kupata ajira, hata nje ya nchi.

Kwa upande wake, ofisa Mawasiliano wa Her Initiative, Daniel Robert amesema mafunzo hayo yatafanyika katika nchi nne za Afrika, ambazo ni Tanzania, Malawi, Ivory Coast, na Zambia, kwa lengo la kuwafikia wajasiriamali 300,000.

“Mafunzo haya yatawalenga wajasiriamali pekee. Tunatarajia kuwafikia vijana 1,500 katika kipindi cha miezi sita kwa kila nchi. Her Initiative na Sheria Kiganjani tutahakikisha malengo haya yanafanikiwa,” amesema Robert.

Celine Julius, mshiriki wa mafunzo hayo, amesema mafunzo yamekuwa msaada mkubwa kwa wajasiriamali kwani sasa wataweza kuandika barua za kazi, kutumia barua pepe, na kujiamini wakati wa mahojiano. Pia watajifunza kutumia mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa zao.

“Mafunzo haya ni msaada mkubwa kwa vijana. Sasa tunaweza kuandika wasifu bora na kutumia barua pepe ipasavyo. Tunajua jinsi ya kujiamini na kutumia mitandao ya kijamii kutangaza kazi zetu,” amesema Julius.

Julius ameongeza kuwa amefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wanawake walioshiriki mafunzo hayo na kuwataka vijana kuchangamkia fursa pale zinapojitokeza.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Isaya Richard, amesema mafunzo hayo yamebadili mtazamo wake kuhusu kutafuta kazi na kumwezesha kufahamu jinsi ya kuandika barua za kazi kwa ufasaha na kuchagua kazi zinazofaa.

“Mafunzo haya yamenisaidia sana. Sasa najua jinsi ya kutafuta kazi sahihi na kufanikisha mahojiano. Mafunzo haya yamebainisha umuhimu wa kuwa na mtaji wa mahusiano na kujua fursa zilipo,” amesema Richard.

Richard amesema kuwa vijana wengi hufeli kwa sababu wanapomaliza chuo hulinganisha elimu yao na hali halisi ya maisha mitaani.

Amesisitiza kuwa ili kufanikiwa, ni muhimu kujenga mtandao wa watu wanaoweza kukuelekeza kuhusu fursa mbalimbali.

Related Posts