Mtwara. Wanafunzi 20 walimu wawili na dereva wamejeruhiwa katika ajali iliyohusisha ya basi la shule na gari la Jeshi la Wananchi (JWTZ) katika eneo la Magomeni, njia ya kutokea Newala kwenda mjini Mtwara.
Wanafunzi hao pamoja na walimu wao walikuwa ni wa Shule ya Msingi Salem na walikuwa wakitoka uwanja wa ndege kujifunza kwa vitendo.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman amesema hali za majeruhi zinaendelea vizuri, isipokuwa mmoja ambaye wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Ligula.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa gari la jeshi lilikuwa linalipita gari moja na kukutana na basi la shule.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, Dk Zawadi Bwanali amethibitisha kuwapokea majeruhi 23 wa ajali hiyo.
Amesema muda wa saa 1 usiku, majeruhi hao walifika katika hosptali hiyo kupatiwa matibabu ambapo majeruhi tisa waliruhusiwa na 14 waliendelea na matibabu, mmoja akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao, Mariam Kombo amesema alipata mshtuko baada ya kupewa taarifa ya ajali hiyo iliyojumuisha watoto wake wawili.
“Nilipokea hizi taarifa kwa mshituko kwa kuwa wanangu wawili walikuwa katika gari hilo, lakini kwa sasa wako salama japo wana majeraha, mmoja ameumia kichwani na mkononi, mwingine kama vile kachanganyikiwa, bado tunasubiri vipimo tujue,” amesema Kombo.
Naye Sophia Kazumali, amesema wajukuu zake wawili walikuwepo kwenye ajali hiyo ambapo mmoja anaonyesha amepata maumivu ya kifua na mwingine ameumia goti.
“Mimi nilikuwa nyumbani nikapigiwa simu juu ya ajali hiyo, nikakimbia kuja hospitalini. Kwa kweli wanaendelea vizuri japo kuna wakati unawaona wana maumivu, hata inafikia wakati tunaongea kwa ishara lakini tunaelewana,” amesema.