Dar es Salaam. Ili kupunguza changamoto ya kuchelewa na upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa makandarasi wazawa wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara nchini, Benki ya CRDB imeanzisha hatifungani ya miundombinu ikienga kukusanya Sh150 bilioni.
Mbali na faida za kimundombinu, hatifungani hiyo inayoanza kuuzwa leo hadi Januari 17,2024, inatoa fursa kwa kila Mtanzania zikiwamo taasisi na kampuni kuwekeza kiasi chochote kuanzia Sh500,000 huku akitarajia kupata faida ya asilimia 12 kwa mwaka.
Hatifungani iliyopewa jina la ‘Samia Miundombinu Bond’ imezinduliwa leo, Novemba 29, 2024. Rais Samia Suluhu Hassan alinunua hatifungani yenye thamani ya Sh200 milioni huku Makamu wa Rais, Dk Philip Isdory Mpango akiwekeza Sh100 milioni, wateja, taasisi na kampuni zilizohudhuria hafla hiyo wamewekeza Sh37 bilioni kwenye hatifungani hiyo.
Akizungumza leo Ijumaa Novemba 29,2024 katika uzinduzi wa hatifungani hiyo, Mkurugenzi Mtendaji CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema fedha zitakazopatikana zitaelekezwa kwenye malipo ya makandarasi wanaoendelea na watakaokuwa wanajenga miundombinu ya barabara nchini kote.
“Pamoja na jitihada nyingine ambazo tumewahi kuzifanya kuwawezesha makandarasi wazawa, leo hii tunajivunia kwa mara nyingine kuja na hatifungani maalum ya upatikanaji fedha kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya barabara ambayo imeidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Fedha na Mitaji (CMSA),” amesema Nsekela.
Mkurugenzi huyo amesema wamekuja na ubunifu huo kwa kuwa wanafahamu Serikali imekuwa ikitenga mabilioni ya shilingi kwa ajili ya ujenzi na kuzirekebisha barabara zilizoharibika ambapo kwa namna moja au nyingine, matumizi ya dharura yamekuwa yakichangia kuchelewesha malipo ya makandarasi.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Philip Mpango, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo akimwakilisha Rais Samia Suluhu, aliwapongeza CRDB na Tarura kwa ubunifu huo na kusema utasaidia kukuza na kuchochea mwitikio wa wawekezaji na Taasisi zingine kutumia chanzo hicho cha fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye gharama kubwa.
“Rais Samia anaahidi Serikali kuendelea kushirikiana na CRDB na taasisi zingine zote za fedha na sekta binafsi kwa ujumla kutatua changamoto za maendeleo katika taifa letu kwani serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara ili kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali,” amesema Makamu wa Rais.
Akielezea hali ilivyo ya mtandao wa barabara nchini, amesema umeongezeka kutoka kilometa 13,235 mwaka 2020 hadi ku kufika kilimeta 15,366 mwaka huu 2024 huku bajeti ya Tarura ikiendelea kuongezeka kutoka Sh414.5 bilioni mwaka 2019/2020 hadi kufika Sh841.2 mwaka 2025/2025.
Pamoja na jitihada hizo, Mpango amesema mahitaji ya kitaifa ya barabara bado ni makubwa kwa kuzingatia ukubwa wa nchi, mahitaji ya kukuza uchumi na kuboresha huduma za jamii bila kusahau ongezeko kubwa la idadi ya watu.
“Hivyo hatifungani inayozinduliwa inalenga kuiwezesha Tarura mtandao wa barabara kwa kuwashirikisha wawekezaji wa ndani katika ugharamiaji wa maendeleo na hususani miundombinu ili kukuza ushirikiano na sekta binafsi na kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa barabara zinazosimamiwa na Tarura unafanyika kwa wakati,” amesema Dk Mpango.
Ameeleza kuwa taarifa zilizoko hadi kufika Machi 2024 Tarura ililazimika kutumia takribani Sh50.43 kukabiliana na uharibifu mkubwa wa barabara ambayo ni zaidi ya mara mbili ya lengo la Sh21 bilioni.
Dk Mpango amezihimiza taasisi mbalimbali ikiwemo Vikoba, kampuni, taasisi zikiwemo za dini, mifuko ya hifadhi ya jamii, mwananchi mmojammoja kuwekeza katika mfuko huo kwa kuwa ni fursa adhimu ya uwekezaji.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa, amesema ujio wa hatuifungani hiyo, ni katika maagizo waliowahi kukaa na Tarura na kuwataka wafikiri kwa kina ili kupata fedha za kukabiliana na ufinyu wa bajeti.
Mchengerwa amesema ujio wake utasaidia kuondoa changamoto zilizopo, huku akiitaka Tarura kuhakikisha wanazisimamia vizuri fedha ambazo watakuwa wanapatiwa.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Albert Chalamila, amesema fedha hizo zitasaidia katika kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiasi kikubwa ikiwemo Jiji la Dar es Salaam, ambalo ni kitovu cha biashara.
Awali Mtendaji Mkuu wa Tarura, Victor Seff, amesema kuanzishwa kwa hatifungani hiyo ambayo ni mahususi kwa ajili ya barabara za wilaya, ni mwendelezo wa utatuzi wa changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa utekelezaji wa jukumu lao la msingi.
Majukumu hayo ni pamoja wa usimamizi, ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara za wilaya zenye jumla ya kilomita 144,429.77 ikiwa ni pamoja na madaraja 3,560 na makalavati 80,326.
“Katika utekelezaji huu, changamoto kubwa tuliyo nayo ni pamoja na ufinyu wa bajeti lakini pia ucheleweshaji wa malipo ya makandarasi wanapokuwa wamekamilisha kazi na hivyo kushindwa kuwalipa kwa wakati kulingana na mikataba tuliyoingia nao’’ amesema.