Na. Damian Kunambi, Njombe
Zaidi ya Lita 200 za mafuta ya petrol na diesel yametolewa bure kwa magari mbalimbali na madereva bodaboda baada ya mkuu wa Wilaya ya Ludewa Olivanus Thomas kuzindulia kituo kipya cha mafuta Wilayani Ludewa Mkoani Njombe kinachomilikiwa na Imani Haule ambaye ndiye mmiliki wa Kampuni ya Kuambiana Investment.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo kwa changamoto ya uhaba wa huduma ya nishati ya mafuta Wilayani humo iliyosababishwa na uhaba wa vituo vya kujazia mafuta ambapo kulikuwa na kituo kimoja pekee ambapo baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakinunua mafuta kwa wingi pindi yanapofika na baadae kuyauza kwa bei ya juu pindi kituoni yanapoisha.
Akizungumza wakati akifanya uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya hiyo Olivanus Thomas amempongeza Imani Haule kwa uwekezaji huo kwani utasaidia kukuza uchumi wa Wilaya hiyo, kutoa ajira na kuboresha huduma ya mafuta hivyo ametoa rai kwa wenye tabia ya kuhifadhi mafuta kwenye madumu Kisha baadae kuyauza kwa bei ya juu kuacha mara moja tabia hiyo kwani kwa atakaye bainika atamchukilia hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Hiki kituo ni msaada mkubwa kwa wanaludewa na hasa watumishi vyombo vya moto, changamoto ya uhaba wa mafuta ilikuwa haiwakanili wananchi pekee Bali hata Serikali kwani mara nyingine tumekuwa tukikwama kwenda mahali mbalimbali kutoa huduma za kiserikali kutokana na mafuta kutopatikana”.
Aidha Kwa upande wake mmiliki huyo wa kituo hicho Imani Haule amesema kituo hicho kimefanikiwa baada ya kupewa wazo na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Sunday Deogratius ambapo alimsihi kuanzisha kituo hicho ili kupunguza changamoto wanayoipata hivyo aliupokea ushauri huo na kuufanyia kazi.
Ameongeza kuwa katika uwekezaji huo amejipanga vyema na atahakikisha huduma inapatikana siku zote na kwa masaa 24 hivyo amewaomba viongozi na wananchi kwa ujumla kumpa ushirikiano wa kutosha.
Hata hivyo uzinduzi huo ulihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi wa Siasa viongozi wa dini pamoja na wananchi.