Mhandisi Besta afichua siri ya ushindi tuzo za NBAA

Utendaji kazi ulijokita kwenye weledi na kusimamia misingi ya taalamu ndio imetajwa kuiwezesha Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), kufanya vizuri kwenye tuzo ya uwasilishaji bora wa taarifa za kifedha iliyotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta wakati akizungumza kwenye hafla ya kupokea tuzo hiyo iliyofanyika usiku wa Novemba 29, 2024 jijini Dar es Salaam.

Amesema uongozi na wafanyakazi wa TANROADS wamekuwa mstari wa mbele katika kufuata weledi na kwamba, tuzo hiyo ni ushahidi wa utendaji bora wa taasisi hiyo kwenye utayarishaji wa taarifa za fedha kwa kufuata viwango vya kitaifa na kimataifa.

“Ni furaha kubwa kwetu kama taasisi inayofuata viwango na weledi kupata tuzo hii. Hii inadhihirisha TANROADS inavyofuata vigezo muhimu vya utayarishaji wa taarifa za kifedha zinazokidhi viwango vya ndani na vya kimataifa,” amesema Mhandisi Besta wakati akipokea tuzo ya mshindi wa pili katika kundi la mawakala wa Serikali.

Hata hivyo, ameahidi kuwa kwa sasa taasisi yake imejipanga kupanda hadi nafasi ya kwanza mwaka 2024 kwa kuimarisha zaidi utayarishaji wa taarifa za kifedha na kuwapatia mafunzo wahasibu wake.

Katika kufanikisha mkakati huo wa kuwa kinara wa tuzo hizo kwa mwaka 2024, Mhandisi Besta amesema wataendelea kufanya kazi kama timu na kuongeza mafunzo kwa waatalamu wake wa fedha.

TANROADS ni moja ya wakala za Serikali inayosimamia miradi mikubwa ya miundombinu nchini, hivyo inatambua umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika utunzaji wa fedha za umma.

Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa TANROADS, Henry Mwakibete, amesema taasisi hiyo imeshika nafasi ya pili kati ya saba zilizoshiriki kwenye kundi la mawakala wa Serikali.

Mwakibete amebainisha kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa TANROADS kushiriki mashindano hayo, jambo linaloongeza uzito wa ushindi huo.

“Sababu kubwa kushika nafasi ya pili ni uwajibikaji na kujitoa kwa watendaji wetu pamoja na kuwa na mafunzo kwa wahasibu wetu na kufuata miongozo ya viwango vya kimataifa,” amesema Mwakibete na kuongeza: Miaka 10 iliyopita, idara ya uhasibu ya TANROADS ilikuwa na wahasibu sita wenye, lakini sasa tuna zaidi ya wahasibu 30 waliothibitishwa. Hawa wanashiriki mafunzo ya mara kwa mara kuhusu uandaaji wa taarifa za za fedha kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Naye Gift Gacharo, ambaye ni mhasibu wa TANROADS Mkoa wa Kagera, amesema mkoa huo umechangia mafanikio ya taasisi hiyo kwa kuandaa taarifa bora za kifedha ambazo hujumuishwa katika ripoti ya jumla ya TANROADS.

“Tumekuwa wa pili katika taasisi za umma zinazotumia IPSA. Tutaendelea kufanya kazi kama timu na tunaamini kuwa mwakani tutakuwa wa kwanza,” amesema Gacharo.

Kwa mwaka 2023, taasisi 86 zilikaguliwa na kushiriki katika tuzo za uandaaji wa hesabu bora. Tuzo hizi hutolewa kwa taasisi zinazokidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa katika uandaaji wa taarifa za fedha na kihasibu.

Masharti muhimu ya kushinda tuzo hizi ni pamoja na taasisi kuwa imesajiliwa na NBAA, hesabu zake kuwa zimekaguliwa na kupewa hati safi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Related Posts