Dk Chana: Tafiti na mitalaa ya chuo itatue changamoto za wananchi

Moshi. Serikali imekiagiza Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori – Mweka kuhakikisha kinaimarisha mitalaa ya tafiti za kitaalamu zinazotolewa chuoni hapo, ili kujibu changamoto zinazoikabili sekta ya uhifadhi na utalii nchini ikiwemo migogoro baina ya wanyamapori na binadamu.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Malisasili na Utalii, Dk Pindi Chana leo Novemba 30, 2024 wakati akizindua bodi mpya ya magavana wa chuo hicho, uzinduzi uliofanyika katika chuo hicho ambacho kipo Kijiji cha Mweka, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Ili kuhakikisha chuo hiki kinaendelea kubaki na hadhi yake kama kituo cha mafunzo ya taaluma ya wanyamapori na utalii ndani na nje ya nchi, naielekeza bodi ihakikishe inaimarisha tafiti zake na ushauri wa kitaaluma kwa lengo la kujibu changamoto zinazoikabili sekta ya uhifadhi na utalii ndani na katika nchi za kikanda,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, Dk Chana amekitaka chuo hicho, kuandaa kozi maalumu itakayozingatia matumizi ya teknolojia katika kulinda maeneo ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori.

“Ili kufaidika na ukuaji wa teknolojia, chuo hiki kiandae kozi maalumu mahsusi zitakazozingatia matumizi ya teknolojia kwenye usimamizi wa wanyamapori na utalii. Sasa hivi lazima tulinde maeneo yetu kwa kutumia mfumo wa kidigitali,” amesema Chana.

Waziri Chana amekipongeza chuo hicho kwa kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 857 mwaka 2022/2023 hadi wanafunzi 1,120 mwaka 2024/2025.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa chuo hicho, Profesa Yunus Mgaya amesema bodi hiyo, itahakikisha inaandaa mitalaa na tafiti zitakazojibu changamoto zinazoikabili sekta ya maliasili na utalii.

“Tutahakikisha tunapitia upya mitalaa yetu ili kuhakikisha utatuzi wa changamoto mbalimbali za uhifadhi na maliasili na utalii zinatatulika, pamoja na kuendeleza maeneo ya mafunzo kwa vitendo na kufanya vizuri katika utoaji wa taaluma zetu,” amesema.

Naye, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Jafari Kideghesho amesema wataendelea kuzalisha wataalamu wa kutosha katika kulisaidia Taifa kupambana na changamoto mbalimbali za kiuhifadhi.

Related Posts