Dk Mpango, vigogo CCM walivyomzungumzia Ndugulile

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amemzungumzia aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, kwa kukumbushia nyakati ngumu walizopitia ikiwamo kuhojiwa na kamati za Bunge.

Dk Ndugulile alifariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27 nchini India alikoenda kwa ajili ya matibabu.

Akitoa  nasaha mbele ya waombolezaji na familia ya Ndugulile iliyowasili Dar es Salaam kutoka Nzega, Dk Mpango amesema Dk Ndugulile alikuwa msaada mkubwa katika kamati hizo kuitetea Serikali.

“Akiwa Naibu Waziri wa Afya, mimi nilikuwa Waziri wa Fedha katika mazingira magumu na wakati mwingine tulikuwa tunabanwa kweli lakini  Dk Ndugulile alishika msimamo kutetea hoja za Serikali,” amesema Dk Mpango.

Dk Mpango amewashukuru wote waliomhudumia Dk Ndugulile kwa upendo katika kipindi ambacho hakuna mtu alikuwa anatarajia.

“Binafsi nilikuwa naye Arusha kwenye mkutano wa mawaziri wa afya wakati akigombea nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kwa Kanda ya Afrika,  ni mwema kweli na watu wote walisema sasa tumepata kiongozi muhimu anayetoka Tanzania,” amesema.

Dk Mpango amesema matumaini ya Serikali ilikuwa kuanzia Februari mwakani kutakuwa na Mtanzania katika nafasi ya Ukurugenzi, Dk Ndugulile alifanya kazi vizuri nimeshuhudia baada ya kufanya naye kazi.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, akimfariji mjane, watoto, ndugu na jamaa wa aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile wakati alipofika kuwapa faraja familia hiyo.

Dk Mpango amesema Dk Ndugulile alikuwa rafiki wa kila mtu labda achokozwe, alikuwa mwema na kama kungelikuwa na uwezo basi tungemuambia Mwenyezi Mungu aturudishie kidogo.

“Tunashukuru kwa maisha yake aliyotuachia na kila mtu anapaswa kujifunza. Tujifunze kuishi vema na ndugu zake kwa kuwa alibaki yeye kama baba wa familia na tunapaswa kujifunza maana kila hatua tunayopiga tunaelekea hukohuko huwezi jua na mimi naongea hapa dakika zangu zimekaribia,” amesema.

Dk Mpango katika maelezo yake ameusia kujenga utamaduni wa kukumbukana pale watu wanapopitia magumu na hata matamu kwa kuwa  Watanzania wana  jadi ya kushirikiana.

“Ninawashukuru wote kwa kujitokeza hapa lakini nataka niwaambie Novemba 27 ilikuwa siku ngumu kwangu nilikuwa kanisani asubuhi. Nilipotoka nilikuta simu mbili zimenitafuta moja ilikuwa inatoka Ofisi ya Rais kunijulisha Dk Ndugulile amefariki dunia,” amesema.

Dk Mpango amesema simu ya pili ilikuwa kutoka kwa rafiki yake ambaye aliwahi kusoma naye na kufanya naye kazi na ni msajili wa hazina naye alifariki siku hiyo asubuhi.

“Sisi kama binadamu tunafundishwa sehemu mbalimbali katika maandiko matakatifu tunaambiwa ya kwetu ni 70 ingawa sikuhizi hata ukienda makaburini unasema mmmh kumbe hata uhai na miaka tunayoishi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu,” amesema.

Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini, Steven Wasira amesema kiongozi huyo alikuwa mzalendo na aliyekuwa anajali zaidi maslahi ya Taifa.

“Niwaeleze tu kwa ufupi misimamo yake wakati mwingine ilikuwa inasababisha kupishana na wakuu wa nchi; alikuwa kiongozi mzuri,” amesema.

Awali Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtevu,  amesema Dk Ndugulile alikuwa ndugu rafiki kwake na anakumbuka wakati anatoka Nzega mwaka 2006 alikokuwa Mkuu wa Wilaya kuja kugombea ubunge, alimuunga mkono.

Amesema ushirikiano huo uliendelea na mwaka 2010 waliingia wote bungeni na kuanza mkakati wa kuomba Kigamboni ipate wilaya.

“Tulikuwa tunashirikiana vizuri na alikuwa mtu wa karibu sana, ingawa yeye hakuwa machachari kama wengine bungeni, Jambo kubwa tulilofanya ni kuja na wazo la kutaka Kigamboni ipate wilaya,” amesema.

Amesema baada ya kuja na wazo hilo walifunga safari hadi kwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho kuomba na hatimaye aliridhia ombi na kuwapa Wilaya ya Kigamboni.

“Dk Ndugulile alikuwa kiongozi mzuri na kupitia taaluma yake ya udaktari mkoa ulikuwa unanufaika. Na hata kichama alikuwa anatoa ushirikiano mzuri,” amesema Mtevu.

Related Posts