Chadema yaweka kiporo ajenda ya uchaguzi

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeiweka kiporo ajenda ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwenye kikao chake cha Kamati Kuu kilichofanyika Novemba 29, 2024 kwa njia ya mtandao.

Badala yake kimeamua ajenda ya uchaguzi huo uliofanyika Novemba 27, ijadaliwe Jumatatu Desemba 2 kwa wajumbe wa kamati hiyo kukutana ana kwa ana jijini Dar es Salaam.

Imeelezwa lengo ni kutoa nafasi kwa viongozi hao kuijadili kwa uzito wake.

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kilifanya kikao cha kamati kuu kwa njia ya mtandao kufanya tathmini ya mwenendo wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ambayo kwa mujibu wa matokeo yalionyesha CCM kimeshinda kwa asilimia 99, Chadema na vyama vingine wakiambulia chini ya asilimia moja.

Kufuatia matokeo hayo ambaye yamelalamikiwa na vyama na makundi mbalimbali, jana Novemba 29, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alisema ushindi huo umetokana na mambo manne – maandalizi mazuri, migogoro vyama vya upinzani, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, utatuzi wa kero za Watanzania pamoja na uratibu mzuri wa kampeni.

CCM ikitamba na ushindi huo, kamati ya uongozi ya Chama cha ACT-Wazalendo jana ilitoa taarifa ya awali ya uchaguzi huo ikieleza kutoridhishwa na mwenendo wake na kutaka ubatilishwe na kurudiwa upya.

Miongoni mwa kasoro zilizojitokeza wakati uchaguzi ukiendelea ni karatasi za kura zilizopigwa kukutwa mitaani, kura kupigwa nje ya utaratibu, wananchi kukosa majina, mawakala kuzuiwa na vifo vya watu watatu katika maeneo tofauti.

Hata hivyo, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema uchaguzi huo uliohusisha vijiji 12,333, vitongoji 64,274 na mitaa 4,269 ulikwenda vizuri kwa asilimia 98 na maeneo ya changamoto yaliyobainika yaliongezewa muda wa saa mbili kutoka saa 10.00 hadi saa 12.00 jioni ili kumaliza kupiga kura.

Kikao cha jana cha kamati kuu ya Chadema kilichoshirikisha viongozi wakuu, akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kilitarajiwa kitoe tamko kwa umma kuhusu kilichoazimiwa kuhusu mwenendo wa uchaguzi huo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Novemba 30, 2024, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema kikao hicho cha kamati kuu kitaendelea Desemba 2.

“Jana (Novemba 29), hatukumaliza tutaendelea Jumatatu, tutakutana Dar es Salaam. Kikao cha dharura ajenda yake ni moja tu ya tathmini ya hali ya uchaguzi wa serikali za mitaa,” amesema Mrema.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Chadema zinaeleza kikao hicho kilichoanza mchana na kuahirishwa jioni, pia kilipokea taarifa za hali ya kisiasa za kanda 10 za chama hicho.

Inaelezwa baada ya taarifa hizo, wajumbe walishauri suala uchaguzi wa serikali za mitaa kulingana na uzito wake, lijadiliwe ana kwa ana.

Baadhi ya wajumbe wa kamati kuu waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina, wamesema kutokana na changamoto za kimtandao na uzito wa kilichotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kikao kifanyike kwa wajumbe kukutana sehemu moja.

“Ilitakiwa kifanyike kesho, lakini kutokana na umbali walipo baadhi ya wajumbe, ikaamuliwa kifanyike Jumatatu ili kuhakikisha wanaotoka mikoa ya mbali wanahudhuria,” amesema mmoja wa wajumbe hao.

Mjumbe mwingine amesema: “Kikao kiliahirishwa kwa sababu ajenda hazikufika mwisho, hasa suala la uchaguzi serikali za mitaa halijajadiliwa kutokana na uzito wake, ajenda ya uchaguzi ni kubwa sana, inahitajika kujadiliwa ana kwa ana,” amesema.

Katika kikao cha Jumatatu, wajumbe wa kamati kuu ya Chadema wataangazia yaliyojiri kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Chama hicho mara kadhaa kimelalamika kuwa licha ya wagombea wake kuenguliwa, mawakala kuondolewa na kura bandia kupenyezwa, makada wake watatu wameuawa.

Related Posts