Ofisi ya Msajili wa Hazina yang’ara tuzo za NBAA

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina imeibuka mshindi wa pili wa tuzo ya umahiri katika uaandaji wa taarifa ya fedha kwa mwaka 2023 katika kundi la Wizara na Idara nyingine za Serikali.

Tukio la ugawaji wa tuzo zilizoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), lilifanyika usiku wa Ijumaa, Novemba 29, 2024.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini – Mashirika ya Kibiashara, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki alisema tuzo hiyo ni matokeo ya uongozi thabiti wa Msajili wa Hazina, Bw Nehemiah Mchechu.

“Mafanikio haya yasingepatikana bila ya muongozo thabiti wa Msajili wa Hazina,” alisema Bi. Mauki baada ya hafla ya ugawaji tuzo iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa APC, uliopo Mbweni— Bunju, Dar es Salaam, kilometa 1.5 kutoka Barabara ya Bagamoyo.

Sanjari na hili, aliongeza, ushindi huu ni matokeo ya mshikamano ndani ya Ofisi ya Msajili wa Hazina—kuanzia Msajili wa Hazina, Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi, Menejimenti na Watumishi wote.

Alisema kutokana na kufanya kazi kwa timu, kumekuwa na utunzaji mzuri wa kumbukumbu za mahesabau katika Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Matumizi mazuri ya kifedha yanachagiza taasisi kuwa na hesabu nzuri za kifedha. Malengo yetu kama Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kuona tunafanya vizuri zaidi ya hapa,” alisema Bi. Mauki.

Related Posts