Dar es Salaam. Baadhi ya wafanyabiashara wenye mizigo iliyokuwa kwenye ghorofa lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, Kariakoo wameingia hofu ya kupoteza mali zao.
Hata hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Toba Nguvila amesema shughuli ya kuwarejeshea wafanyabiashara mali zao inaratibiwa na kamati maalumu, hivyo wote wataipata.
Jengo la ghorofa nne liliporomoka Kariakoo Novemba 16, 2024 likisababisha vifo vya watu 31, huku wengine 88 wakiokolewa.
Baada ya kuporomoka jengo hilo ambalo pia lilitumika kama stoo, mizigo ya wafanyabiashara ilikusanywa na kwenda kuhifadhiwa ikielezwa utaratibu maalumu utatumika kuichukua.
Wakizungumza na Mwananchi leo Novemba 30, 2024 baadhi ya wafanyabiashara wamelalama kwamba kuna changamoto ya usimamizi wa mizigo, huku wengine wakidai yao imepotea au kuchukuliwa isivyo halali na watu wengine.
Mmoja wa wafanyabiashara aliyezungumza kwa sharti la kutokutajwa jina, amesema amepata mizigo yake baada ya kueleza alama ya utambulisho.
“Nimepata mizigo yangu, tulikuwa tunaeleza code (alama ya utambulisho) imekuwa rahisi kwa baadhi yetu ambao tulikuwa tunaeleza mizigo yetu ilivyo na hatukupata shida,” amesema.
Yahaya Mamboleo, ambaye ni kuli amesema bosi wake amepata mizigo yake lakini si yote.
“Hapa kuna mizigo ya jengo lililoanguka na lile lililoangukiwa kwa hiyo wote wamefika sehemu ambayo imehifadhiwa mizigo unakuta watu wawili wanataja mzigo mmoja,” amedai na kueleza kutokana na sintofahamu hiyo, utoaji mizigo umesitishwa.
Asha Salim, mfanyabiashara wa nguo za kike amesema walipoambiwa kutakuwa na utaratibu maalumu, walijua wataitwa kwa kutumia majina waliyoandikisha awali.
“Niliambiwa mizigo yote imepelekwa jeshini kwa usalama, lakini nilipofika huko nikakuta baadhi ya bidhaa zangu hazipo. Inaonekana watu walichukua mali ambazo si za kwao,” amelalamika Asha.
Mfanyabiashara aliyekuwa na ghala la mizigo kwenye ghorofa hilo, Shukurani Mwakalindile amesema ni muhimu kwa Serikali kuweka mifumo madhubuti ya kuhifadhi mali za watu katika matukio ya dharura.
“Hali kama hii inaweza kuzua matatizo makubwa ikiwa hakutakuwa na mfumo wa uwazi na uwajibikaji, maana watu wanakwenda pale hakuna majina zaidi ya kuonyesha mzigo wako kwa hiyo mtu anaweza kuchagua chochote,” amesema.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, kutokana na kuwapo malalamiko walitakiwa kuonyesha mkataba wa upangaji wa jengo lililoporomoka.
“Ili kuepusha mgogoro uliojitokeza walianza kudai mikataba, wafanyabiashara hawakuwa nayo wengine walisema wamepoteza, huku wengine wakiwa hawana kabisa,” amesema mfanyabiashara mwingine.
Amesema baadhi ya waliofika kuchukua mizigo majina yao ni tofauti na yaliyopo kwenye mikataba ya pangishaji wa jengo.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, kila mmoja ana namna yake iliyomwezesha kupata fremu ya duka katika eneo hilo.
“Wapo wanaowajua wenye nyumba wao, wengine wamepangishwa na madalali na wanawalipa hao na wengine wamepangishwa na watu ambao walikodi fremu kwa wahusika ndiyo maana wengi wao hawawajui wenye nyumba,” amesema Jeremia Swai, mfanyabiashara wa vitenge.
Amesema tatizo hilo linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa linapotokea tatizo wasijue wa kumfuata ili kupata haki yao kwani kuna mzunguko mrefu katika upangishaji wa maeneo ya biashara.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Nguvila amesema shughuli ya kuwarejeshea wafanyabiashara mali zao linaratibiwa na kamati maalumu.
“Serikali, polisi, usalama wa Taifa, Takukuru wote wako pale nani atachukua mzigo usio wake?” alihoji.
Amesema kamati inayoratibu utoaji wa mali hizo na kuwarejeshea wamiliki ina muunganiko wa vyombo vyote, ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, mhasibu wa jiji, kitengo cha manunuzi cha jiji, na Ofisi ya Waziri Mkuu, ambao wote wako hivyo kila kitu kitakwenda sawa.
Amesema mizigo iliyookolewa kwenye ghorofa lililoporomoka Kariakoo haipo sehemu moja, imehifadhiwa kwenye sehemu tofauti.
“Ile ya waliokuwa na stoo mizigo yao ipo sehemu nyingine na ya wale wafanyabiashara wadogo ipo kwenye ‘godown’ (bohari) jingine lipo bandarini, na huko huenda haijaanza kutolewa,” amesema Nguvila.
Kuhusu mizigo hiyo awali kupelekwa kwenye kambi ya jeshi amesema ilipelekwa kwa ajili ya kuchambuliwa ili kuweka vizuri.
“Katika jengo kulikuwa na vitu tofauti kama fedha na vitu vya thamani na vinginevyo, hivyo vilipelekwa Lugalo kuchambuliwa vipi ni vipi,” amesema.
Akizungumzia kuhusu michango ya maafa, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk Jim Yonazi amesema pamoja na kwamba shughuli za uokoaji zimefikia tamati, mfuko wa maafa unaendelea.
“Michango ya mfuko wa maafa inapokewa muda wote hata kama hakuna maafa, inapotolewa inatunzwa ikitokea dharura inatumika,” amesema Yonazi.
Kuhusu maswali yaliyopo mtaani iwapo fedha zinazokusanywa kwenye mfuko wa maafa zitasaidia kuwapunguzia hasara wafanyabiashara walioathiriwa, Yonazi amesema Serikali bado inalifanyia kazi.
“Tukikamilisha hili tutasema,” amesema Yonazi alipozungumza na Mwananchi.
Awali, Serikali iligharimia maziko ya watu waliopoteza maisha katika jengo hilo.