Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Geita imemnyima ruhusa ya kukata rufaa nje ya muda, mfungwa Deogratius William, mkazi wa Geita anayetumikia adhabu ya kifungo jela, kwa makosa ya ubakaji na kusambaza virusi vya Ukimwi na Ukimwi.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo katika shauri la maombi ya mfungwa huyo alilolifungua akiomba kuruhusiwa kukata rufaa nje ya muda, kutokana na kushindwa kutoa sababu za msingi za kuchelewa kukata rufaa hiyo.
Deogratius alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Geita kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa kosa la ubakaji na miaka mitano kwa kosa la kusambaza virusi vya Ukimwi katika kesi ya jinai namba 57/2023.
Katika kesi hiyo, Deogratius alishitakiwa kwa makosa mawili ubakaji kinyume cha vifungu vya 130 (1) na (2) na 131A (1) na (2) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyorekebishwa mwaka 2022.
Katika shtaka la pili alishtakiwa kwa kosa la kusambaza virusi vya Ukimwi na Ukimwi kinyume na kifungu cha 47 cha Sheria ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi ya mwaka 2008.
Mahakama ya Wilaya katika hukumu yake ya Januari 17, 2024 ilimtia hatiani kwa makosa yote mawili na kumhukumu kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kwanza la ubakaji na miaka mitano kwa kosa la pili la kusambaza virusi vya Ukimwi na Ukimwi.
Deogratius hakuridhika na hukumu hiyo, lakini alijikuta amechelewa kukata rufaa ndani ya muda uliowekwa kisheria, hivyo alifungua shauri la maombi akiomba ruhusa ya kukata rufaa hiyo nje ya muda.
Katika shauri hilo alitoa sababu mbili, kwanza akidai kuwa alikuwa anasubiri nakala za hukumu na mwenendo na sababu ya pili alidai kuwa aliugua ugonjwa ambao ulimfanya ashindwe kukata rufaa hiyo.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Kelvin Mhina Novemba 28, 2024, imemkatalia mfungwa huyo maombi yake baada ya kujiridhisha kuwa hakukidhi matakwa ya kisheria, kwa kushindwa kutoa sababu za kuiridhisha za kuchelewa kukata rufaa hiyo.
Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Deogratius ambaye alijiwakilisha mwenyewe, aliieleza Mahakama kuwa baada ya kuhukumiwa adhabu na kupelekwa gerezani, aliugua na kulazwa hospitalini ambako alifanyiwa upasuaji wa ngiri.
Aliongeza kuwa baada ya kuruhusiwa na kupona kabisa ndipo akafungua shauri hilo.
Wakili wa Serikali Deodatha Dotto alipinga rufaa hiyo akidai kuwa mwombaji alishindwa kuwasilisha ushahidi kwamba alikuwa mgonjwa na alifanyiwa upasuaji, kwani hakuwasilisha cheti cha matibabu kuthibitisha madai yake na wala hakutaja hospitali alikotibiwa.
Akijibu hoja hiyo Deogratius alidai kuwa cheti cha matibabu kiko gerezani.
Kuhusu suala la kupewa nakala ya hukumu na mwenendo Wakili Dotto, alisema kuwa mwombaji alishindwa hata kuambatanisha nakala hizo kuthibitisha madai ya kwamba alipewa nakala hizo Aprili 30, 2024.
Alisema kwa kuzingatia kifungu cha 14 (1) cha Sheria ya Ukomo na msimamo wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa kesi moja na akaeleza kuwa mwombaji ameshindwa kutoa sababu za kuridhisha.
Jaji Mhina katika uamuzi wake akirejea uamuzi wa kesi nyingine ya Mahakama ya Rufani, amesema kuwa Mahakama hiyo imeweka vigezo vinne vya kuzingatia katika shauri la maombi kama hilo katika kuruhusu kukata rufaa nje ya muda ikiwemo ugonjwa.
Hata hivyo, amesema kuwa lazima kuwepo ushahidi na maelezo ya dhahiri namna gani ugonjwa huo ulimzuia mwombaji kuendesha kesi yake.
Amesema kuwa katika shauri hilo si kwenye kiapo wala kwenye mawasilisho ya mwombaji ambako imeoneshwa kuwa baada ya hukumu hiyo Januari 17, 2024 ni lini aliugua na lini alipona, ili kujua kama ugonjwa huo ulimzuia kuchukua hatua muhimu ndani ya muda.
Pia amesema kuwa ilikuwa ni muhimu mwombaji huyo kutoa ushahidi wa cheti cha matibabu kuthibitisha kuugua na kulazwa na kufanyiwa upasuaji, lakini hakuweza kuwasilisha ushahidi huo.
“Hivyo sababu ya ugonjwa inakosa mashiko,” amesema Jaji Mhina.
Kuhusu sababu ya kusubiri nakala ya hukumu na mwenendo, Jaji Mhina amesema kuwa mwombaji hakuweka katika kiapo au kuwasilisha ushahidi wowote kuwa alipewa nakala hizo Aprili 30, 2024.
Pia amesema kuwa hata kama ni kweli alipewa nakala hizo Aprili 30, 2024, swali ni kwamba kwa nini alifungua shauri hilo la maombi ya kuongezewa muda Oktoba 31, 2024 (miezi sita baadaye baada ya kupewa nakala hizo).
Hivyo Jaji Mhina amesema kuwa msimamo wa sheria katika kesi mbalimbali zilizokwishaamriwa na Mahakama kuwa ikiwa mtu atachelewa kuchukua hatua inayostahili, mwombaji anapaswa kuelezea kila siku mojamoja aliyochelewa.
Pia mwombaji ameshindwa kutolea maelezo kwa kila siku aliyochelewa kutoka pale ambapo muda wa kukata rufaa uliisha.
“Kwa hiyo, mwombaji alishindwa kutoa sababu nzuri na za kuridhisha kuhalalisha mahakama hii kutumia busara zake kuridhia kuongeza muda. Matokeo yake nalitupilia mbali ombi hili”, amesema Jaji Mhina.