USAID Afya Yangu na Kizazi Hodari Kanda ya Kusini kutoa huduma za VVU kwenye maadhimisho ya kuelekea siku ya Ukimwi duniani.

Miradi ya USAID Afya Yangu na Kizazi Hodari Kanda Ya Kusini inayofadhiliwa na Shirika la Msaada Kutoka Watu wa Marekani na kusimamiwa na Deloitte Consulting Limited imejipanga vyema ili kutoa huduma za VVU wakati wa maadhimisho ya kuelekea siku ya Ukimwi duniani ambayo kitaifa yatafanyika Mjini Songea mkoa wa Ruvuma Jumapili Disemba mosi.

Akizungumza Mjini Songea kwenye uwanja wa Maji Maji ambapo ndio kunafanyika maandalizi ya kuelekea kilele cha siku hiyo, Mshauri Mwandamizi wa Huduma za Ukimwi na Kifua Kikuu kutoka Mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini George Sikalengo alisema kuwa wamejipanga vyema kuhakikisha kuwa wanatoa huduma za VVU kwa jamii na sana sana kwa vijana wakati huu wa kuelekea kwenye kilele cha siku ya Ukimwi Duniani.

‘Sisi mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini tumekuwa tumekuwa tukisaidia upatikanaji wa huduma bora na rafiki za Ukimwi na kifua kikuu kwa jamii kwenye mkoa huu wa Ruvuma. Hata hivyo, kwenye wiki ya kuelekea kwenye maadhimisho ya ukimwi Duniani tumejipanga vizuri na kuongeza juhudi Zaidi kuendelea kutoa huduma za VVU kwa wananchi ambao wanajitokeza kwenye uwanja huu wa Maji Majji Mjini Songea’, alisema Sikalengo.

Sikalengo aliongeza, ‘Kwa hapa tunatoa huduma za upimaji pamoja na kuunganisha wananchi wanaopatikana na virusi vya VVU kwenye kliniki za tiba na matunzo (CTC), huduma endelevu za tiba yaani dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi, huduma shirikishi za kifua kikuu, upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi, huduma za uzazi wa mpango pamoja na rufaa za huduma wa wahanga wa ukatili wa aina mbalimbali.

Vile vile tunatoa huduma za elimu ya mabadiliko ya kitabia kwa jamii kwa lengo la kuwaongezea uwezo wa jamii kufika katika vituo vya afya na kuomba huduma, alisema Sikalengo huku akiongeza kuwa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini pia wanaongeza  uwezo wa jamii kutambua wahitaji wa huduma na kuwahamasisha kujiunga/kwenda kupata huduma husika.

Maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani kwa mwaka 2025 kitaifa yatafanyika Jumapili Disemba Mosi, Songea mkoani Ruvuma na kauli mbiu ya mwaka huu inasema ‘Chagua njia sahihi tokomeza UKIMWI’ huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango akitarajiwa kuwa mgeni Rasmi.

Related Posts