RAIS MSTAAFU DKT. KIKWETE AWAPA POLE NA KUWAFARIJI WANA FAMILIA WA MAREHEMU DKT. FAUSTINE NDUGULILE

Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mhe. Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Mchinga jioni ya leo Jumamosi Novemba 30, 2024 wamefika Kigamboni jijini Dar es salaam kutoa pole na kufariji wana familia ya Marehemu Dkt. Faustine Ndugulile, aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Afrika aliyefariki dunia Jumatano iliyopita nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Dkt Kikwete na Mama Salma walipofika nyumbani kwa marehemu walitoa mkono wa pole kwa mama mzazi wa marehemu, mjane, ndugu, jamaa, marafiki na mahirani waliofika msibani hapo. Miongoni ya watu waliokuwepo wakati huo walikuwa mwanasiasa mkongwe mzee Stephen Wassira na Mbunge wa Viti Maalum Mhe Halima Mdee.

Dk. Ndugulile, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 55 aliwahi kuwa waziri mdogo wa Afya, na amefariki dunia miezi mitatu tu baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo, akitarajiwa kuanza rasmi majukumu yake Februari mwakani.

Alichaguliwa kuwa Mkuu wa Kanda wa WHO, akichukua nafasi ya Dk. Matshidiso Moeti wa Botswana, ambaye alihudumu kwa vipindi viwili vya miaka mitano.

Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema alikuwa “ameshtushwa na kusikitishwa sana” na kifo cha Dk. Ndugulile. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pia alituma salamu za rambirambi.


Picha na ISSA MICHUZI






Related Posts