Kamisheni ya maafa yatahadharisha matumizi ya umeme, gesi

Unguja. Kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar imesisitiza jamii kuchukua tahadhari ya matumizi ya nishati ya umeme na gesi kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.

Kauli hiyo imetolewa na ofisa mawasiliano na tahadhari za mapema kutoka Kamisheni hiyo, Rahma Vuai Suleiman wakati akitoa elimu kwa wajumbe wa kamati za sheha katika shehia za Mkoa wa Mjini Magharibi, Novemba 30, 2024.

Bila kutaja takwimu, amesema baadhi ya ajali za moto zinasababishwa na matumizi mabaya ya majiko ya umeme na gesi, hivyo kuiathiri jamii kukosa makazi. Amewataka wazazi na walezi kuwasimamia watoto wao wanapotumia nishati hizo.

“Ipo haja ya kuzingatia matumizi ya nishati na gesi ili kuepusha tatizo la majanga ya moto yanayoepukika,” amesema.

Amesema katika msimu wa mvua za vuli kumejitokeza majanga mbalimbali yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko kwa baadhi ya maeneo hasa ya mabondeni, mlipuko wa maradhi ya matumbo, upepo mkali unaosababisha athari mbalimbali.

Ofisa Maafa Wilaya ya Mjini, Pili Haji Foum ametaka kuwapo mikakati ya kukabiliana na maafa katika shehia na kuziorodhesha sehemu zote hatarishi zilizopo katika maeneo yao.

Amesema iko haja ya jamii kubadilika kutokana na mazingira yaliyopo ya mifumo ya umeme ya kizamani badala yake itumike ya kisasa.

“Wananchi wanapaswa kuzima vifaa vya moto baada ya kumaliza matumizi ili kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza na kuleta athari kwa jamii,” amesema.

Akitoa mafunzo ya matumizi sahihi ya majiko ya gesi, Abdullah Hussein Hamad kutoka Kampuni ya Ismail LPG, amesema iwapo majiko na gesi vikitumika vyema havina madhara na ni salama kuliko nishati nyingine za mkaa na kuni.

Sheha wa Shehia ya Mtumwajeni, Rajab Ally Ngauchwa amesema ipo haja ya kutoa elimu, akiwataka wajumbe hao kushirikiana kuwahudumia wananchi na kutoa taarifa mapema zinapojitokeza changamoto ndani ya shehia zao.

“Elimu hii ni nzuri tunapaswa kupambana na majanga haya, elimu inabidi iendelee kutolewa ili kukomesha matatizo haya,” amesema.

Related Posts