WAHITIMU MWEKA WATAKIWA KUWA WAZALENDO KULINDA RASILIMALI ZA NCHI

 

Na Happiness Shayo- Kilimanjaro

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amewataka Wahitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori MWEKA kuwa wazalendo kulinda rasilimali za nchi huku wakitumia elimu na ujuzi bora walioupata kufikia malengo yao.

Ameyasema hayo katika Mahafali ya 60 ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori MWEKA yaliyofanyika leo Novemba 30, 2024 Mkoani Kilimanjaro.

Pia, Mhe. Chana amekitaka Chuo hicho kuwa wabunifu kwa kufanya tafiti zitakazotatua changamoto kama migogoro ya binadamu na wanyamapori, viumbe vamizi, mabadiliko ya tabia nchi na magonjwa ya wanyamapori, mifugo na binadamu.

“Nimefarijika kusikia changamoto ya udahili wa wanafunzi wa nje, ikiwemo Msumbiji, imetatuliwa. Naipongeza Bodi ya Magavana na Menejimenti kwa hatua hii muhimu inayodumisha hadhi ya Chuo kama kituo bora cha mafunzo ya wanyamapori na utalii Afrika, sambamba na kukuza utengamano wa kikanda (au regional integration) na kubadilishana utaalamu na uzoefu” amesema Mhe. Chana.

Katika hatua nyingine Mhe. Chana amesema Wizara ya Maliasili na Utalii inaunga mkono wazo la kuanzisha Kampasi ya Chuo hicho nchini Msumbiji, hatua itakayokuza diplomasia, undugu wa kihistoria na hadhi ya kimataifa ya Chuo.

“Nimefurahi pia kusikia Chuo kimeanza kutekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, alilolitoa Agosti 27,2024, wakati anafungua kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi za wakurugenzi na watendaji wakuu wa taasisi za umma ambapo alizielekeza taasisi na mashirika ya umma kuangalia fursa za kibiashara na utoaji huduma  nje ya Tanzania” ameongeza Mhe. Chana. 

Aidha, amesema Chuo hicho  kione uwezekano wa kushirikiana na nchi ama taasisi nyingine zenye mahitaji ya mafunzo kwa lengo la kuwajengea watumishi wao uwezo katika fani za uhifadhi na utalii. 

Naye Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Jafari Ramadhani Kideghesho, alisema kuwa jumla ya wahitimu 505 wamehitimu mafunzo katika taaluma mbalimbali za wanyamapori na utalii na kwamba Chuo hicho kimezalisha wataalamu takribani 12,000 kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika huku  asilimia 70 wameajiriwa  katika taasisi mbalimbali za uhifadhi.

Ameongeza kuwa chuo hicho kinatoa mchango makubwa kwenye uhifadhi wa wanyamapori na kwamba mitaala imejielekeza kujibu changamoto sugu za uhifadhi ikiwemo kukabiliana mabadiliko ya tabianchi na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori MWEKA, Prof. Yunus Daud Mgaya amewapongeza wahitimu kwa nidhamu, kujituma, kufuata maelekezo na kufikia mafanikio kuhitimu chuo hicho huku akisisitiza kuwa mojawapo ya mikakati ya Chuo hicho ni kufanya tafiti kuzalisha taarifa mpya na kutoa utatuzi wa changamoto za kiikolojia, kijamii, kiuchumi na pia kuimarisha miundombinu na vitendea kazi ili watumishi wafanye kazi kwa ufanisi.

Related Posts