Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Faustine Ndugulile, alikuwa rafiki yake huku akieleza namna alivyojitosa kusaka kura ili aishike nafasi hiyo mpya.
Kikwete amesema hayo baada ya kufika nyumbani kwa Dk Ndugulile yanakofanyika maombolezo akiwa ameambatana na mkewe Salma Kikwete ambaye ni Mbunge wa Mchinga mkoani Lindi.
Mwili wa Dk Ndugulile aliyefariki usiku wa kuamkia Novemba 27 mwaka huu akiwa nchini India, unatarajiwa kuzikwa Desemba tatu mwaka huu katika Makaburi ya Mwongozo Kigamboni.
Akizungumza nyumbani hapo mbele ya waombolezaji, Dk Kikwete amesema Dk Ndugulile alikuwa anamtumia zaidi kwenye mataifa ambayo yalikuwa hayajaweka bayana msimamo wa kura yao.
“Ghana tulikuwa na mkutano na mawaziri wa afya Afrika nilijitosa kumpigia kampeni ingawaje kipindi hiki sikuwa maarufu sana lakini wengi bado wananikumbuka,” amesema.
Kikwete amesema kwenye nchi kama Serra Leone ambazo hazikuonyesha upande, alikuwa anawapigia simu mawaziri husika moja kwa moja.
“Nilimpigia simu waziri wa Afya wa Sera Lione kumueleza kijana wetu anagombea ..aliniuliza anagombea nini? Nikamjibu anagombea WHO Afrika msimamo wenu haueleweki, basi alinijibu na kunihakikishia kura,” amesema.
Katika maelezo yake Dk Kikwete amesema walitumia mfumo huo kwa baadhi ya nchi.
“Yale maeneo magumu nilikuwa naambiwa na kwa lugha za kimombo za watani wangu hawa nilikuwa nakandamiza tu, basi nikawa naendelea kukandamiza na hatimaye aliposhinda alinipigia simu na nilimtakia kila la kheri,” amesema.
Dk Kikwete amesema kikubwa kumshukuru Mungu kila mtu ana namna yake ya kuja duniani na namna ya kuondoka na kusisitiza kuwa mipango ya Mola hakuna anayeweza kuingilia.
“Tunashukuru kwa Mungu kwa kutupa muda wa kuishi na Dk Ndugulile amefanya mengi mazuri na hayo tutaendelea kuyakumbuka daima. Kufiwa si jambo dogo hasa unapofiwa na mzazi au mzazi anapofiwa na mtoto unayetegemea labda baadaye atakuzika na Dk Ndugulile amefariki akiwa bado kijana miaka 55,” amesema.
Dk Kikwete amesema chimbuko la urafiki wao ni baba yake Dk Ndugulile alikuwa ofisa wake alipokuwa waziri wa mambo ya nje.
“Nimekuja kutoa pole familia ya marehemu Dk Ndugulile, Baba yake alikuwa ofisa wangu nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje, nilikuwa nafahamiana na Ndugulile na hata alipofariki baba yake nilikuja hapa na hii ni mara yangu ya pili bahati isiyokuwa nzuri na kuja kipindi cha majozi,” amesema.
Kikwete amesema wakati anakuja kwenye msiba huo wa baba yake kipindi hicho Dk Ndugulile alikuwa katika hekaheka za kura za maoni, huku akieleza uliibuka uvumi kuwa anamuunga mkono.
“Tatizo la siasa kwa Kiingereza wanasema ‘Perception’ yaani jinsi mtu anavyokufikiria kama mbaya unakuwa mbaya mbaya lakini tukio lililonileta ni kuja kumuona mwenzangu baba yake nilikuwa nafanya naye kazi wizara ya mambo ya nje,” amesema.