Na. Peter Haule, WF,
Dodoma
Serikali imesema kuwa ulipaji
wa madai yanayotokana na kupokelewa kwa bidhaa au huduma huzingatia masharti ya
mikataba ya zabuni au kandarasi iliyoingiwa kati ya Serikali na mtoa huduma.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu
Lameck Nchemba(Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Temeke Mhe. Dorothy George Kilave,
aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuwasaidia wafanyabiashara kulipwa madai na riba
wanapo cheleweshewa malipo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali hulipa au hulipwa
riba iwapo masharti ya mikataba ya zabuni au kandarasi imekiukwa.
Akijibu swali la nyongeza
la Mbunge huyo la kuitaka Serikali kutoa maelekezo ili wazabuni walipwe madai
yao pamoja na riba wakicheleweshewa fedha baada ya kuingia mikataba, Mhe. Dkt.
Nchemba alisema kuwa Serikali inaangalia namna ya kuliweka jambo hilo kwenye
kanuni za ununuzi ili kuwalinda wazabuni wa ndani ambao si tu kwamba
wanacheleweshewa malipo yao, bali pia Wakandarasi kutoka nje wanaoingia nao
mikataba ya kazi huwalipa kwa shilingi ya Tanzania wakati wao wanalipwa kwa dola
za Marekani.
Aidha, Dkt. Nchemba
alisema kuwa Serikali inakamilisha kanunui za ununuzi baada ya Bunge
kurekebisha Sheria ya ununuzi wa umma, lengo ni kuhakikisha wakandarasi wa
ndani wananufaika na kazi wanazozifanya.
Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Mhe. Cosato David Chumi, kuhusu muda ambao Serikali itaanza kurejesha asilimia 20 (Retention) ya Kodi ya Ardhi kwenye
Halmashauri kama ilivyopitishwa katika Sheria ya Fedha 2023/2024, Dkt. Nchemba
alisema kuwa urejeshwaji wa kodi hiyo utaanza baada ya zoezi la
kukusanya kodi ya ardhi litakapoanza kutekelezwa rasmi na Mamlaka za Serikali
za Mitaa.
“Utaratibu wa kurejesha
asilimia 20 ya kodi ya ardhi kwenye Halmashauri unatarajiwa kuanza kabla au
ifikapo Juni 30, 2024”, alisema Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa hadi Aprili
2024, taratibu za kuwezesha halmashauri kuanza kukusanya kodi ya ardhi hazikukamilika
hususan kufungamanisha mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi na mfumo wa
kukusanya mapato ya halmashauri – TAUSI.
Alisema mwaka 2023/24,
Serikali ilifanya maboresho ya ukusanyaji wa kodi ya ardhi ambapo halmashauri
kupitia Ofisi ya Rais -TAMISEMI zinatakiwa kukusanya kodi ya Ardhi kwa
kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali
la Mbunge wa Temeke, Mhe.
Dorothy George Kilave na Mbunge wa Mafinga Mjini, Mhe. Cosato David Chumi, kuhusu
mpango wa Serikali wa kuwasaidia wafanyabiashara
kulipwa madai yao pamoja na riba wanapo cheleweshewa malipo na pia Serikali
itaanza lini kurejesha asilimia 20 (Retention)
ya Kodi ya Ardhi kwenye Halmashauri.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)